Kampuni ya Boeing imetangaza mabadiliko kwenye mfumo wake wa kuzuwia ajali unaohusishwa na ajali ajali mbili za ndege zake za 737 Max zilizosababisha vifokatika kipindi cha miezi mitano.
Lakini bado haijajulikana ni lini ndege hizo zilizozuwiwa kusafiri kote duniani mwezi huu zitaruhusiwa kupaa.
Kama sehemu ya kuboreshandege hizo , Boeing itaweka mfumo wa onyo kulingana na viwango ,ambao awali ulikua si wa lazima.
Ndege zake zilizopata ajali za makampuni ya Lion Air ya Indonesia na Ethiopian Airlines, hazikuwa na mfumo wowote wa kuashiria ajali, ambao lengo lake ni kuwaonya marubani wakati mtambo wa uongozaji wa safari ya ndege unapotoa taarifa kinyume na matarajio.
Boeing imesema makampuni hayatakuwa yakitozwa pesa za ziada kwa ajili ya kuweka mfumo huo wa usalama wa ndege.
Mtengenezaji wa ndege pia amesema atafanyia mabadiliko programu ambao umehusishwa na ajali.
Mfumo wa MCAS , ulioundwa kuzuwia ndege kupoteza mwelekeo , huwa unatambua taarifa za kifaa cha kutambua ikiwa ndege mwinuko wa kasi ya kupindukia au la.
Lakini uchunguzi wa ajali ya ndege ya Lion Air iliyotokea mwaka jana ulionyesha kuwa mfumo huo ulikuwa haufanyika kazi ,na kulazimisha ndege kuelekea chini zaidi ya mara 20 kabla ya kuanguka ndani ya bahari na kuwauwa abiria 189 pamoja na wahudumu.