Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitafungua kesi mahakamani kupinga Sheria ya Vyama vya Siasa Sheria ambayo wamedai ni mbaya kutokana na vifungu vyake kukiuka Katiba, misingi ya utawala bora na mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo Tanzania imetia saini.
Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa leo Ijumaa Machi 22, amesema dhamira yao hiyo iko palepale ambapo wanaendelea kushauriana na vyama vingine na wadau mbalimbali njia nzuri zaidi ya kufungua shauri hilo mahakamani mapema iwezekanavyo.
“Sheria hii imeenda kufanya shughuli za kisiasa nchini kuwa ni jinai kwani kila kifungu cha sheria hii kimeweka adhabu ya faini, kifungo au vyote kwa pamoja kwa wanasiasa, ila Msajili na Serikali na vyombo vyake hakuna kifungu hata kimoja ambacho kinawagusa kama wakikiuka utekelezaji wa sheria hii.
“Mathalani kifungu cha 3 (b), kimempa Msajili wa Vyama vya Siasa jukumu la kusimamia chaguzi za ndani ya Vyama ikiwa ni Pamoja na teuzi za wagombea wa nafasi mbalimbali.
“Hii inampa Msajili mamlaka ya kuingilia vyama na kuviamulia ni nani awe kiongozi wa chama husika au mgombea wa nafasi ya kiserikali kama mgombea urais na ubunge, hii ni kinyume na Katiba ya nchi ambayo imetoa fursa na haki ya kujumuika kwa wananchi wake,” imesema taarifa hiyo.