OBREY Chirwa amewaambia washikaji zake pale Yanga kwamba anatamani kurudi Jangwani ingawa Azam wanamlipa mkwanja mzuri.
Mzambia huyo alikuwa Yanga akatimkia Misri kwa madai kwamba njaa ilizidi lakini Hans Pluijm akamvuta Azam akamwaga wino. Pluijm amepigwa chini akamuacha Chirwa Azam.
Kwa mujibu wa Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, Chirwa amemuendea hewani besti mmoja ambaye ni mchezaji wa kikosi cha kwanza akamwambia anatamani kurudi Yanga.
“Unaona yule Chirwa anayecheza Azam, kule kuna kila kitu lakini amempigia simu mchezaji wangu mmoja ambaye ni rafiki yake akamwambia anatamani kurudi Yanga,” alisema Zahera alipotembelea Ofisi za Global Publishers Sinza Mori, Jijini Dar es Salaam, juzi Jumanne na kuongeza.
“Pale Azam kuna kila kitu lakini mchezaji kama Chirwa alishakuwa na mtandao wa watu wengi, alikuwa ana uwezo wa kufanya mambo yake bila kutegemea mshahara.
“Lakini ilifi ka mahali akajisahau akaondoka Yanga, sasa hivi anawaambia wenzake kwamba pale Azam anaishi kwa kutegemea mshahara tu hakuna zile pesa za pembeni na watu wa Yanga hawawezi kumpa sasa hivi kwavile siyo mchezaji wao.
“Ndio maana niliwaambia wachezaji wangu Yanga hakuna mshahara tuko kwenye hali mbaya, lakini tukishinda tutapata pesa nyingi kuliko mishahara.
“Na kweli kila tukishinda wachezaji wanapata zaidi ya laki mbili, hizi gharama kama za kodi ya nyumba, kulipia luku ni mambo ambayo wanazipata kwa mashabiki wakishinda.” Zahera alisisitiza kuwa kutokana na hela hizo wanazopata wachezaji wake kutoka kwa wadau, ndizo zinawafanya kuzidi kuwa na mzuka.