Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF, Khalifa Suleiman Khalifa amesema chama hicho hakiwezi kufa kwa sasa kutokana na uongozi mpya ambao umeingia madarakani kuwa unaongozwa na Mwenyekiti wake Profesa Ibrahim Lipumba.
Katibu Mkuu huyo wa CUF ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na www.eatv.tv juu ya maoni ya baadhi ya wadau wa siasa ambao wamekuwa wakieleza mitazamo yao tofauti juu ya hatma ya Chama Cha Wananchi CUF, baada ya Maalim Seif kutangaza kuhama.
"CUF haielekei shimoni, bali inaelekea kwenye mafanikio kwa sababu wale wasaliti washaondoka ndani ya chama chetu, kuhusu kushinda Wabunge wengi kwa sasa bado ni mbali sana maana unaweza kuungwa mkono na watu wengi lakini kwenye sanduku la kura ukashindwa", amesema Khalifa.
Khalifa amesema, "sijui wanaposema kuvaa viatu vya Maalim Seif wanazungumzia nini?, kama wanazungumzia kufanya majukumu ambayo alikuwa anafanya, nitahakikisha nitajitahidi kujenga ushawishi kama Maalim Seif japo sijui watachukulia vipi kwa sababu ya fitna na majungu yanayoendelea kupandikizwa", ameongeza.
Hivi karibuni akizungumza na www.eatv.tv, Khalifa alisema katika kuhakikisha CUF mpya inazaliwa ina mpango wa wakushirikiana na baadhi ya viongozi wenzake wa vyama vya upinzani pamoja na Chama Cha Mapinduzi.
Khalifa alisema kuwa, "nikikutana na kiongozi wa CCM, nitamwambia chama ni taasisi ambayo inadhamira ya kujenga nchi yetu, naomba tushirikiane na tusaidiane, ili tupate mafanikio ya vyama vyetu".