Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo amesema yuko mbioni kuwashughulikia matapeli wa misitu ambao wanatumia vibaya jina la Rais Magufuli.
Amesema serikali kamwe haitomvumilia mtu yeyote atakayekutwa akifanya shughuli zozote za kibinaadamu ikiwemo kuchoma rasilimali ndani ya msitu wa hifadhi wa Kazimzumbwi uliopo Kisarawe mkoani Pwani na kwamba yeyote atakayekutwa ndani ya msitu huo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Akizungumza katika uzinduzi wa upandaji miti elfu 20 katika msitu wa Kazimzumbwi unaosimamiwa na WWF, Mkuu huyo wa Wilaya amesema kumekuwapo na matukio ya mara kwa mara ya wananchi kuingia na kuchoma moto msitu huo.
Wengine miongoni mwa wavamizi hao wakiamua kuyachukua maeneo ya msitu huo na hata kuyauza kwa kisingizio kuwa yameidhinishwa na Rais Magufuli.
Naye meneja wa uhifadhi wa misitu WWF Tanzania Saimon Lugandu amesema licha ya mapambano wanayoyafanya ili kuilinda rasilimali misitu lakini bado kumekuwa na tabia ya baadhi ya wananchi kuwa kikwazo kikubwa cha kukwamisha ukuaji wa misitu ndani ya hifadhi.