“SISI wanadamu hatuna lolote katika ulimwengu huu. Kama si leo kesho, kama si kesho, keshokutwa. Huwezi kujua muda gani na siku gani wakati wako utafika, safari yako itakuwa imefika”
Ujumbe mfupi wa video uliorushwa na watu wengi kwenye mitandao ya Facebook, WhatsApp na Instagram juu ya maneno aliyoyasema mtangazaji maarufu wa Clouds Media Group, Ephraim Kibonde.
Kibonde alisema maneno hayo alipohojiwa kuhusu kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba.
Kutokana na maneno hayo na mazingira halisi yaliyopo sasa, inaonyesha kama Kibonde aliashiria kifo chake kwani ni takriban siku nne amefariki dunia tangu kuzikwa kwa Ruge nyumbani kwao Kizuru, Bukoba mkoani Kagera.
Wakati wa msiba wa Ruge, Kibonde alikuwa mshereheshaji tangu Dar es Salaam hadi Bukoba mkoani Kagera. Kwa hakika ni msiba juu ya msiba na ni pigo kwa Clouds Media na tasnia ya habari kwa ujumla kuondokewa na watu wawili chini ya wiki mbili.
Kibonde alifariki dunia alfajiri ya kuamkia jana jijini Mwanza kwa tatizo la shinikizo la damu wakati akiwahishwa Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Bugando kutoka hospitali ya Uhuru jijini humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga, alisema familia ya Clouds imepata pigo lingine kubwa kwa kuondokewa na mfanyakazi wao Kibonde.
Alisema Kibonde alianza kuugua akiwa kwenye msiba wa Ruge na baada ya kuanza kwa matatizo hayo, walifanya jitihada za kumpeleka Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kagera ya Bukoba kwa matibabu.
“Baada ya kupelekwa hospitali ya Bukoba ilionekana kuna umuhimu wa kumpeleka hospitali ya Uhuru iliyoko Mwanza na alifikishwa kwenye hospitali hiyo na kupata matibabu yaliyompa nafuu. Wakati akijiandaa kurudi Dar es Salaam, hali ikabadilika ghafla na kufariki dunia. Taratibu za mazishi zitafanyika nyumbani kwake, Mbezi (Dar es Salaam),” alisema.
Wakati wa mazishi ya Ruge, mtangazaji Kibonde alikuwa miongoni mwa waliokuwa wakitangaza matangazo ya moja kwa moja kutoka kijiji cha Kizuru akionekana mzima wa afya.
Katika shughuli hiyo, Kibonde alikuwa akiongoza makundi mbalimbali yaliyojitokeza siku hiyo kwa kuyataja kwenda kuweka udongo na mashada ya maua kaburini.
Jana asubuhi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, alithibitisha kuwa Kibonde amefariki dunia na kwamba alianza kusumbuliwa na shinikizo la damu alipokuwa Bukoba kwenye msiba wa Ruge na baadaye alihamishiwa jijini Mwanza.
Kibonde ambaye ni mmoja wa watangazaji wa kipindi cha Jahazi cha Clouds FM kinachorushwa hewani kila siku jioni, akiwa na mwenzake Gadna G Habash, alijipatia umaarufu kutokana na ucheshi wake na maneno yaliyojaa vichekesho na vitimbi.
WENGI WAMLILIA
Tangu kutangazwa kwa taarifa za msiba huo jana asubuhi, watu mbalimbali walianza kueleza wanavyomfahamu Kibonde huku wakikumbushia msiba wa Ruge na ule wa mke wake, Sarah, uliotokea mwaka jana.
Katika mtandao wa Instagram moja ya picha iliyotumiwa na watu wengi ni ambayo inamWonyesha Kibonde akimhoji Ruge wakati huo wakiwa vijana.
Kabla ya kumzika Ruge, mtangazaji huyo aliweka picha ya mke wake marehemu Sara Kibonde kwenye ukurasa wake wa Instagram. Watu wengi walichangia kwa kumpa pole ya ‘RIP Sarah’.
Baadhi ya watu walioguswa na msiba huo ni pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ambaye katika ukurasa wake wa Instagram, aliandika: “Poleni sana Clouds kwa pigo hili kubwa! Hakika mnapitia katika kipindi cha majaribu.
“Mungu awatie nguvu. Njia yetu ni moja...pole nyingi kwa familia, ndugu na marafiki wa marehemu. Tunamwombea pumziko la amani ndugu yetu Ephraim Kibonde.”
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Harrison Mwakyembe aliandika Instagram maneno yanayosomeka hivi: "Taarifa za kifo cha mtangazaji mahiri na maarufu nchini, Kibonde wa Clouds, zimenishtua sana. Ni pigo la pili kubwa kutokea katika kipindi kifupi. Si tu kwa Clouds Media bali kwa tasnia nzima ya habari."
Aliendelea kuandika: "Wakati tunasubiri kutoka kwa madkatari kujua chanzo cha kifo chake na vilevile mipango ya mazishi yake, nitumie nafasi hii kuipa pole familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki, wana Clouds Media na wana habari wote kwa ujumla, kwa msiba huu mkubwa. Bwana alitoa, Bwana ametwaa, Jina la Bwana lihimidiwe."
JK ATOA YA MOYONI
Naye Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, aliandika kwenye Twitter akisema: “Majonzi yangali nasi, nimepokea taarifa ya kifo cha mtangazaji Ephrahim Kibonde wa Clouds. Ni pigo kubwa kwetu sisi wapenzi wa kipindi cha Jahazi.”
Kikwete, maarufu kama JK, aliendelea kuandika: “Jahazi litaeleaje bila ya Nahodha Kibonde? Mwenyezi Mungu na aipe faraja familia yake, Clouds na wasikilizaji wote wa Jahazi.”
Mfanyabiashara maarufu, Mohamed ‘MO’ Dewji, katika ukurasa wake wa Instagram aliandika: “Nawawaza watoto wake, wamebaki yatima, Mungu awape nguvu. Pumzika kwa amani Kibonde, Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un.”
Msanii wa bongo Fleva, Judith Wambura, ‘Lady J Dee’ naye aliandika Instagram, “Hili ni jambo zito kwa watu wenye ukaribu na Ephraim Kibonde. Tunakaa tunakunywa, tunacheka siku nyingine mmoja wetu anatwaliwa.”
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi, aliandika kwenye Intagram: “Hakika inatosha kifo kuwa ni mawaidha tosha kwa wanadamu. Kama mpenzi wa kipindi cha Kahazi la Clouds, tutammiss sana brother Kibonde kwa ucheshi, umahiri na kipaji chake cha pekee. Poleni familia na Clouds Media Group.”