Kimbunga Idai kimesababisha uharibifu mkubwa katika baadhi ya maeneo nchini Msumbiji, Malawi na Zimbabwe katika kile ambacho Umoja wa mataifa unasema huenda ni janga baya zaidi la hali ya hewa kuwahi kushuhudiwa kusini mwa Afrika.
Mamilioni ya watu walikuwa kwenye njia ya moja kwa moja na kimbunga hicho huku mji wa pwani wa Beira nchini Msumbiji ukiathirika zaidi.
Idadi ya waliyofariki nchini Msumbiji kufikia sasa ni watu 200 lakini rais Filipe Nyusi anahofia idadi hiyo huenda ikawa juu zaidi.
Watu 100,000 wanahitaji kuokolewa katika mji wa pwani wa Beira (hapo juu), kwa mujibu wa serikali ya Msumbiji.
Mamia ya watu bado hawajulikani walipo huku jamaa zao wakijaribu kupekua vifusi kuwatafuta wapendwa wao.
Katika mto Umvumvu, hapo chini, wakaazi wanangalia kwa mshangao jinsi daraja la kuvuka mto huo lilivyoporomoka.