Wanajeshi wa India na Pakistan wameshambulia vituo vya kijeshi na vjiji kwenye mpaka wao wenye shughuli nyingi za kijeshi wa jimbo linalogombaniwa la Kashmir, katika machafuko mapya licha ya nchi hizo mbili kuongeza juhudi za kutuliza mvutano.
Wanajeshi wa nchi hizo wametuhumiana kwa kuanzisha mashambulizi katika eneo hilo. Hakuna habari zozote zilizotolewa maramoja kuhusu hasara iliyotokea.
Hofu imekuwa kubwa tangu ndege ya India iliporuka katika anga ya Pakistan wiki iliyopita ikifanya kile ambacho India ilisema ni shambulizi dhidi ya wanamgambo waliohusika na mlipuko wa bomu wa kujitoa mhanga Februari 14 katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India, ambalo liliwauwa wanajeshi 40 wa India.
Katika juhudi nyingine za kutuliza mvutano na India, Pakistan jana iliwakamata watu kadhaa akiwemo kaka wa kiongozi wa kundi la wanamgambo lililopigwa marufuku la Jaish e Mohammad, ambalo lilidai kuhusika na shambulizi la bomu la kujitoa muhanga Kashmir.