Jaji Mkuu aagiza kupelekewa mashauri yote ya Mirathi

Jaji Mkuu aagiza kupelekewa mashauri yote ya Mirathi
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma ameagiza kupelekewa mashauri yote ya Mirathi nchi nzima ili aweze kujua ni changamoto gani inayofanya yachelewe kumalizika na kupanga mkakati wa kisheria ili mashauri hayo yawe yanaisha ndani ya muda uliowekwa kisheria.

Akizungumza katika ziara yake ya kikazi aliyoanza mkoani Mtwara, Jaji Mkuu alisema katika mahakama za Mwanzo mashauri hayo yanatakiwa yaishe ndani ya miezi sita lakini yapo mengine yamekaa zaidi ya miaka kumi.

Alisema kutokana na kuchelewa kumalizika kwa mashauri haya, wakati mwingine humfanya msimamizi wa mirathi kuendelea kunufaika na mali za marehemu wakati warithi wapo na wanataabika kwa muda mrefu.

Jaji Mkuu amesema ametoa agizo hilo pia kwa kuwa mashauri ya aina hiyo huweza kuzalisha migogoro mingi katika jamii na kusababisha haki kutokupatikana kwa wakati.

Akizungumzia changamoto nyingine zinazoikabili Mahakama ya Tanzania katika kutekeleza jukumu lake la msingi la utoaji wa haki, Prof. Juma alisema Mahakama inakabiliwa na changamoto kubwa ya wananchi kutofahamu taratibu za kisheria jambo linalosababisha washindwe kupata haki kwa wakati.

Alisema hivi sasa Mahakama ya Tanzania imejiwekea utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya taratibu za kisheria kabla ya kesi kuanza kusikilizwa Mahakamani ili kuwasaidia wanannchi kutambua nini cha kufanya

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama imeamua kuwa wazi katika kutekeleza majukumu yake ikiwa ni moja ya hatua muhimu za mapambano dhidi ya rushwa ndani ya Mhimili huo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad