Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Semistocles Kaijage ametangaza uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki utafanyika Mei 19 mwaka huu.
Jaji Kaijage ameitoa taarifa hiyo leo akiwa mkoani Morogoro ambapo ameeleza kwamba tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Tanzania.
"Nafasi ya jimbo la Arumeru ipo wazi na imetokana na aliyekuwa mbunge Joshua Samwel Nassari kupoteza sifa ya kuwa mbunge kutokana na kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge mfululizo bila ruhusa ya Spika," amesema Jaji Kaijage
Machi 14, 2019 Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alimuandikia barua Mwenyekiti wa NEC, Jaji Kaijage kumtaarifu jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi kutokana na kutohudhuria vikao vya mikutano mitatu mfululizo.
Aidha Mwenyekiti Kaijage amevitaka vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo ya uchaguzi wakati wa kipindi cha uchaguzi mdogo.
Nassari anadaiwa kutohudhuria, mkutano wa 12 wa Septemba 4 hadi 14 mwaka 2018, mkutano wa 13 wa Novemba 6 hadi 16 mwaka 2018 na mkutano wa 14 wa 29 Januari hadi Februari 9 mwaka 2019.