Jopo la Madaktari Mjini London Laeleza Jinsi Lilivyomuondolea Virusi Mtu wa Pili, Aliyekuwa Amethirika na Virusi vya Ukimwi



Jopo la wanasayansi limetangaza kufanikiwa kumuondolea virusi mwathirika wa Virusi vya Ukimwi ama VVU kwa kutumia tiba ya kumpandikiza uboho kutoka kwa mtu ambaye hajaathirika na virusi hivyo. Huyu ni mgonjwa wa pili.


Hiki ni kisa cha pili kilichoonesha mafanikio kama hayo baada ya kile cha kwanza cha mwaka 2007. 

Kwa mujibu wa DW. Madaktari wametumia njia ya kupandikiza uboho ili kuviondoa Virusi vya Ukimwi ama VVU kwa mwathirika mmoja wa virusi hivyo vinavyosababishwa UKIMWI. Ingawa wanasifu matokeo ya utafiti huo, lakini wanaonya kwamba ni mapema mno kumthibitishia kwamba amepona.

Watafiti wametangaza kuwa mtu huyo aliyekuwa ameambukizwa virusi vya Ukimwi sasa yuko katika hali nzuri. Huyu ni mwathirika wa pili wa VVU kufanyiwa matibabu kama haya, aliyepachikwa jina “mgonjwa wa London,”, ambaye amefanikiwa kuondolewa virusi hivyo vilivyowaathiri takriban watu milioni 37 duniani kote.

Mgonjwa huyo, aliiomba timu yake ya matibabu kuficha utambulisho wake.

Matibabu na matokeo yalichapishwa katika jarida la kisanyansi la kimataifa la “Nature” na yanatarajiwa kutangazwa rasmi katika mkutano wa masuala ya tiba utakaofanyika huko Seattle, Marekani siku ya Jumanne.



Wanasayansi walitumia njia ile ile ambayo ilitumiwa na kuonyesha mafanikio kwa mgonjwa wa VVU mjini Berlin, hapa Ujerumani mwaka 2007.

Kiongozi wa jopo la utafiti huo, Ravindra Gupta, alinukuliwa akisema “Kufikiwa kwa hatua hii kunakoonyesha ahueni kwa mgonjwa huyu wa pili na kulikotokana na mbinu ileile iliyotumiwa awali, kunatokana na mgonjwa wa kwanza wa Berlin kutoonyesha shida yoyote.”

Katika visa vyote viwili, wagonjwa walipandikizwa uboho kutoka kwa watu waliokuwa na uwezo wa kuhimili VVU. Lakini pia alisema, kubadilisha chembehai za mwathirika na watu hao kumeonekana kumwezesha mgonjwa kuzuia virusi vya Ukimwi kurejea baada ya matibabu.
 .

Kulingana na Gupta, mgonjwa wa London aligunduliwa na VVU mwaka 2003 na amekuwa katika  tiba ya kudhoofisha makali ya virusi vya Ukimwi tangu mwaka 2012, ARV. Tiba huyo hudhoofisha tu virusi hivyo na si kuviondoa. Alifanikiwa kupandikizwa uboho mnamo mwaka 2016, lakini akiendelea kutumia tiba kwa muda wa miezi 16 kabla ya kuacha matibabu hayo. Na tangu hapo,  hajaonesha dalili yoyote za kuwa na virusi kwa miezi 19 sasa.

Amesema hawajaona virusi hata baada ya kumpima. Hata hivyo, alionya kwamba “ni mapema mno kusema kwamba amepona.”

Mtafiti huyo alisema mafanikio haya ya mara ya pili ya kuviondoa Virusi vya Ukimwi kwa kutumia njia hiyo ya kupandikiza uboho itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa tafiti za kimatibabu, lakini akisisitiza kuwa upandikizaji huo wa uboho ambao ni hatari, unaouma na wenye gharama kubwa, hauwezi kuwa chaguo bora zaidi la matibabu ya VVU.

Ni asilimia 59 tu ya watu wanaoishi na VVU duniani kote wanapata ARV. Watu milioni moja hufa kila mwaka kutokana na magonjwa yanayohusiana na VVU na UKIMWI. Karibu watu milioni 35 wamekufa kutokana na UKIMWI tangu kuanza kwake miaka ya 1980.

By Ally Juma.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad