Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai, amemuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya taifa ya uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage, kumtaarifu kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki lililokuwa likiongozwa na Joshua Nassari liko wazi.
Kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi ya ya Bunge kitengo cha mawasiliano na uhusiano wa Kimataifa, imesema kuwa Nassari amepoteza sifa za kuwa Mbunge kutokana na kitendo cha kutohudhuria vikao vitatu vya Mikutano ya Bunge.
"Uamuzi huo wa Spika umezingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 71 (1)(c). Ibara hiyo inaeleza kuwa, Mbunge atakoma kuwa Mbunge au ataacha kiti chake Katika Bunge ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya Mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika", imesema taarifa hiyo.
Vikao vilivyomponza Nassari
Nassari hajahuduhuria Mkutano wa kumi na mbili wa tarehe 4 hadi 14 Septemba 2018, mkutano wa kumi na tatu wa tarehe 6-16 Novemba 2018 na mkutano wa kumi na nne wa tarehe 29 Januari hadi 9 February 2019.Nassari akiwa kwenye moja ya kikao na viongozi wa CHADEMA jimboni kwake