Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Wizara ya Madini kwa utekelezaji wa Ujenzi wa Jengo la Taaluma la chuo cha Madini Dodoma (MRI) na Ujenzi wa Jengo la Ofisi za Wizara ya Madini lilipo eneo la Mji wa Serikali Ihumwa, Jijini Dodoma.
Hayo yamesemwa Machi 13, 2019 na Wajumbe wa Kamati hiyo wakati wa kikao cha majumuhisho kilichofanyika kwenye jengo la wizara ya Madini Ihumwa, mara baada ya kukagua majengo yote mawili na kupewa taarifa ya ujenzi wake.
Wakiwa kwenye jengo la taaluma la chuo cha madini, wajumbe wamepongeza na kuridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa na kupongeza SUMA JKT kujenge jengo hilo.
Jengo la Taaluma ni la ghorofa tatu lenye ofisi, vyumba vya kufundishia na ukumbi wa mikutano. Ujenzi huo utagharimu jumla ya shilingi 2, 863, 161, 369.00 hadi kukamilika kwake na unatekelezwa chini ya chini ya Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Raslimali Madini (SMMRP) kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Akizungumzia ujenzi wa jengo la Wizara, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amewaeleza wajumbe wa kamati kuwa, ujenzi huo ulianza tarehe 4/12/2018 na ulitakiwa kukamilika tarehe 31/01/2019, hata hivyo mkandarasi hakuweza kukamilisha ndani ya muda huo kutokana na sababu mbalimbali. Prof. Msanjila ameongeza kuwa, kwa kuzingatia ushauri wa msimamizi wa ujenzi huo, walifikia makubaliano ya kumuongezea muda mkandarasi hadi kufikia tarehe 28/02/2019.
Prof. Msanjila ameongeza kuwa, mpaka sasa ujenzi huo umefikia asilimia 80 na mwezi ujao wizara itakuwa tayari kuhamia. Amesema ujenzi huo umegharimu Jumla ya shilingi Milioni 975,360,028.10 zitatumika katika ujenzi huo.
Naye, Waziri wa Madini Doto Biteko ameiambia kamati kuwa, mkandarasi wa ujenzi huo, alipewa muda wa mwezi mmoja kukamilisha ujenzi wake ili wafanyakazi wa Wizara hiyo waanze kulitumia. Waziri emeleza kuwa wizara inaridhishwa na kasi ya mkandarasi katika ujenzi huo.
Biteko ameongeza kuwa, wizara imedhamiria kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na kuthibitisha hilo wizara imemteuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Raslimaliwatu, Nsajigwa Kabigi ambae yupo muda wote wote eneo la ujenzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dunstan Kitandula amesema pamoja na wabunge kuipongeza wizara kwa kazi nzuri, ameishauri wizara na mkandarasi wa ujenzi huo, Mzinga Holdings Company kujielekeza kwenye manunuzi ya vifaa vinavyopatikana hapa nchini.
Wakichangia wajumbe wa kamati hiyo, Joseph Musukuma na Ally Keissy wakichangia wakati wa majumuhisho waliipongeza wizara na mkandarasi, hata hivyo, walishangaa muda waliopewa na hatua iliyofikia, msukuma alisema ni kazi ya kupongeza na wameeleza pamoja na mkandarasi kutokamilisha kazi yake kwa wakati bado utendaji wake wa kazi unaridhisha na kasi yake inaonekana.
Naye, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo aliwaambia wajumbe wa kamati kuwa, ujenzi wa jengo hilo la wizara unafanana ramani na wizara nyingine ikiwemo kiasi cha fedha zilizotolewa na serikali zote zikiwa na kiwango cha shilingi Bilioni moja.
Amesema muda uliotolewa ulilenga kutimiza azma ya wizara kuhamia eneo hilo kwa wakati. Aliwashukuru wajumbe kwa ushauri wao na kueleza kwamba kama wizara watauzingatia.