Kangi Lugola aliliwa Kondoa, ‘Baba tusaidie na hawa polisi’
0
March 03, 2019
Jeshi la polisi wilayani Kondoa mkoani Dodoma linatuhumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu sanjari kuligeuza jeshi hilo kama duka kwa kuwatoza wananchi fedha ili kuwaachia pindi wanapoona waliowakamata hawana makosa.
Sakata hilo limeibuka wiki mbili ziliopita baada ya kufanya msako wa nyumba kwa nyumba na mitaani kukamata wananchi na wengine wakiwa wanafunzi wa shule kwa madai ya kufanya vitendo vya uhalifu maarufu kama (Panya road).
Wakizungumza na wanahabari wilayani humo baadhi ya wananchi wamesema kuwa sakata hilo na mengine mengi ndiyo yanawafanya kumuomba waziri wa mambo ya ndani ya nchi Kangi Lugola kuitembelea wilaya hiyo kwenda kusikiliza kero zao.
kwa upande wake Mohammed Omari mkazi wa Ubembeni amesema kuwa hawapingi zoezi la kuwakamata watu ila wanachopinga ni ulaji rushwa wa jeshi hilo kwani amedai kuwa wamewageuza kuwa ni mitaji.
Amesema kuwa kimsingi jeshi hilo wilayani humo limekuwa la kibiashara zaidi kuliko kulinda usalama na mali za raia hivyo wamewaomba viongozi wanaosimamimia jeshi hilo kwa dhati kwenda kujionea na kusikiliza kilio chao.
“Utaona watu wamekaa takribani siku tano bila dhamana halafu wanaenda mahakamani na kufunguliwa kesi ya uzururaji hapa utaona kimsingi jambo hilo kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria za mtuhumiwa”amesema Omari.
Naye Mkazi wa Kigamboni Salama Ibrahim amesema kuwa vijana wake walifuatwa nyumbani usiku majira ya saa saba usiku na kuchukuliwa kwenda polisi hali ambayo walijikuta wakifunguliwa kesi ya uzururaji na hadi leo kesi hiyo ipo mahakamani na Jumatatu watasomewa hukumu baada ya kupigwa kalenda tokea jumatatu ya wiki hii.
Tags