Katibu wa Bunge, Ndugu Stephen Kagaigai amekanusha taarifa zinazodai kuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amesamehewa na kurejeshewa ubunge wake, ikiwa ni siku kadhaa tangu Spika wa Bunge kusema kuwa amepoteza sifa.
Kagaigai akizungumza na www.eatv.tv, amesema kuwa hakuna taarifa za namna hiyo akiwa kama Katibu wa Bunge hakuna kingine anachoelewa zaidi ya Mbunge huyo kukosa sifa za kuendelea kuwa Mbunge.
Mwandishi: Hallow Mheshimiwa habari za kazi, unazungumza na Mwandishi kutoka www.eatv.tv.
Mh. Kagaigai: Karibu kuna nini tena?
Mwandishi: Kuna taarifa zinazungumzwa mtandaoni kuwa Nassari amesamehewa na kurejeshewa Ubunge wake.
Mh. Kagaigai: Amesamehewa? Kwani amelikosea nini Bunge?
Mwandishi: Ni baada ya ile barua iliyoandikwa na Spika kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC, ikiitaarifu kuwa jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi na kutokana na Mbunge aliyekuwepo kupoteza sifa.
Mh. Kagaigai: Hapana hakuna taarifa kama hizo, hilo ndio nasikia kwako.
Kwa upande wake Nassari baadaya kutafutwa na www.eatv.tv, alidai kuwa hajui lolote na anachojua ni kuhusiana na Mahakama, tayari shauri liko Mahakamani linalozuia jimbo lake kufanyiwa uchaguzi.