Kiama Chaja kwa Waliolipa kodi ya pango la ardhi ya nyumba

Kiama Chaja kwa Waliolipa kodi ya pango la ardhi ya nyumba
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ameanzisha kampeni maalumu ya kuwasaka wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi ya nyumba kwa nyumba na wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi ambao hawajalipa hadi mwaka huu.

Kampeni hiyo ambayo aliizindua mwishoni mwa wiki wilayani Karatu mkoani Arusha, alipokuwa akisikiliza na kutatua migogoro ya ardhi ya wakazi wa wilaya hiyo katika kampeni ya Funguka kwa Waziri, amewaagiza watendaji wote wa wilaya na kanda nchini kuanza kuwasaka nyumba kwa nyumba wadaiwa wa kodi ya ardhi.

“Naagiza mikoa yote ya Tanzania Bara kuanza kampeni rasmi ya kuwasaka wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi ya nyumba kwa nyumba na msiwaonee huruma hata kama ni waziri na anadaiwa kodi ya ardhi peleka mahakamani hata kama ni kiongozi yeyote, hata kama Mkuu wa Wilaya mfuate na peleka mahakamani," alisema Waziri Lukuvi.

Aliwataka wamiliki wote wa ardhi kujitathmini na kukagua taarifa zao kama wamelipa kodi ya ardhi na kuanza kulipa haraka kabla kampeni hiyo haijamfikia mdaiwa.

Aliwataka watendaji wake wasiwe na huruma na mtu yeyote anayedaiwa kodi kwa sababu fedha za kodi ndizo zinazosaidia katika ujenzi wa miundombinu na utoaji huduma kwa wananchi na ndizo zinazosaidia uendeshaji wa serikali kwa kiasi kikubwa.

Alisema kila mtu aliyemilikishwa ardhi kwa matumizi yoyote lazima alipe kodi kwa wakati isipokuwa tu wale ambao wamesamehewa kuanzia mwaka huu wa fedha na Rais na Bunge limeridhia kwamba maeneo ya kuabudu na maeneo ya kutolea huduma bila biashara kama vile shule, zahanati, misikiti na makanisa na taasisi zisizofanya biashara zisilipe kodi hiyo.

Waziri Lukuvi pia aliwaagiza wenyeviti wote wa mabaraza ya ardhi na nyumba ambao wanahusika na hukumu za masuala ya ardhi, kusimamia na kuzipa kipaumbele kesi zote za watu wanaoshtakiwa kwa kutokulipa kodi ya pango la ardhi na kuzichukulia kwamba ni kesi kubwa katika kipindi hiki.

Alitaka kesi zote za wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi zitolewe hukumu kwa siku moja na mtu atozwe faini siku hiyo hiyo na akishindwa kulipa, hati yake ibatilishwe au kupigwa mnada kwa nyumba au mali yake kufidia kodi anayodaiwa.

Aidha, Waziri Lukuvi aliwaagiza maofisa ardhi wote kupekua mashamba yote ambayo yanatumika kwa biashara yanayolimwa na yenye hati yalipe kodi na kama hawatolipa basi watafutiwa hati zao kwa kuwa kigezo kikubwa cha kufutiwa hati ni kutokulipa kodi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad