Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Prof. Ibrahim Haruna Lipumba ametuma salamu kwa Katibu Mkuu wa chama hicho kuwa aende ofisini ili ampatie kazi.
Prof. Lipumba ametuma salamu hizo leo, kupitia mkutano na waandishi wa habari wakati akiielezea sintofahamu ya awali ya mkutano wake kuzungukwa na vyombo vya usalama, huku CUF upande wa Maalim Seif wakiwa wameweka pingamizi mahakamani.
Wanahabari walipotaka kujua kutoka kwa msajili ni kwa sababu gani Mkutano huo umeruhusiwa kufanyika wakati kukiwa na zuio la Mahakama, Naibu Msajili ambaye alihudhuria mkutano huo alidai kwamba, "ofisi yangu haitambui upande, inatambua viongozi wa kitaifa na ndiyo hawa waliopo hapa".
Baada ya jibu hilo, Lipumba aliongeza kuwa,"Kwa kuwa huwa unazungumza nae, mueleze Maalimu, aje hapa Buguruni nimpangie kazi, akishafika hapa nitampangia kazi atajua nini cha kufanya".
Akitoa sintofahamu ya kwamba Mkutano wao ulizingirwa na vyombo vya usalama, Lipumba alisema kwamba Mkutano huo ni halali na unaendelea na hautakuwa na matatizo, "polisi wamekuja kuweka ulinzi ".
Mbali na hayo Naibu Msajili wa vyama vya siasa amesema kwamba amehudhuria mkutano huo kwa kuwa ni halali na unatambulika kutokana na Katiba ya Chama cha CUF na hata kama asingealikwa bado angehudhuria kwa kuwa sheria mpya ya vyama vya siasa inamruhusu kufanya hivyo.