Lugola atoa onyo kali kwa wanaoingiza wahamiaji haramu nchini

Lugola atoa onyo kali kwa wanaoingiza wahamiaji haramu nchini
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ametoa onyo kali kwa baadhi ya Watanzania ambao wanafanya biashara ya kuwaingiza wahamiaji haramu nchini huku wakijua kufanya hivyo ni kinyume na sheria za nchi.

Kutokana na changamoto hiyo, Waziri Lugola amesema Idara ya Uhamiaji itashirikiana na Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwakamata watu hao na kuwafungulia mashtaka.

Akizungumza mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, kumaliza kukagua eneo la ujenzi wa Makao Makuu ya Uhamiaji, jijini Dodoma, leo, Lugola alikiri uwepo wa wahamiaji haramu nchini, na akasisitiza kuwa tatizo la uwepo wa wahamiaji haramu litamalizika.

“Naomba muwafikishie salamu watu ambao wanatabia hiyo ya kuwaingiza wahamiaji haramu nchini, Serikali ipo na pia inafanya kazi, kama wapo basi wajue tutawakamata tu,” alisema Lugola.

Alisema Jeshi la Polisi litashirikiana na Uhamiaji kuwatafuta popote wahamiaji hao walipo, na watakapokamatwa watafikisha ujumbe kwa wenzao wenye nia ya kuja nchini kwa njia isiyo halali.

Aidha, Lugola aliwataka Suma JKT wanaojenga jengo la Makao Makuu ya Uhamiaji wafanye kazi kwa weledi mpaka jengo hilo litakapo kamilika, na pia mara kwa mara viongozi wa Wizara yake akiwemo yeye mwenyewe atakuwa anatembelea eneo hilo la ujenzi.

“Sitasubiri mpaka Mheshimiwa Rais haje hapa kukagua, litalifuatilia mwanzo mwisho ujenzi huu, na pia mlisema pale Magereza Ukonga mbele ya Rais, kuwa Jeshi halishindwi, nami ninaamini nyie Suma JKT, ujenzi huu utakamilika bila kuwa na matatizo,” alisema Lugola.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu, alisema ujenzi huo unatarajiwa kwenda vizuri na pia endapo watapata changamoto zozote wawe huru wajenzi hao kuja kumuona kwasababu ofisi za Wizara zipo jirani na eneo la ujenzi huo na pia naye atakua anautembelea mradi huo.

Naye Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala, alisema ujenzi wa jengo hilo kubwa wa ghorofa nane kwenda juu na moja kuja chini, ukikamilika litakua la kisasa, na ukubwa wa jengo hilo utawasaidia kufanya kazi zao kwa utulivu zaidi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad