WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewaagiza Makamanda wa Polisi nchini washirikiane na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuchunguza na kuwakamata wapinzani wanaomtukana Rais pamoja na Serikali kwa ujumla kupitia vikao vyao vya ndani vya siasa.
Akizungumza na mamia ya wananchi wa Mjini Kilosa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Kilosa Town, Wilayani humo, juzi, Lugola amesema ana taarifa kuna baadhi ya wapinzani ambao wanafanya vikao vyao vya ndani huku wakitukana, kubeza pamoja na kuwachonganisha wananchi na Serikali yao ambayo inaongozwa na Rais Dkt John Magufuli.
Kutokana na wapinzani hao kuvunja agizo lililowekwa, amewaagiza Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wilaya nchini kuwachunguza viongozi wa siasa kwa kina kupitia vikao vyao, na watakaowabaini wanavunja utaraibu huo wawakamate haraka iwezekanavyo.
Lugola ameendelea kusisitiza kwa kupiga marufuku kufanyika kwa mikutano ya siasa ya hadhara mpaka hapo kampeni zitakapoanza rasmi kwa uchaguzi ujao.
“Mimi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sitakubaliana na kiongozi wa chama chochote kuvunja agizo tulilolitoa nchi nzima kwa kutokuruhusu kufanyika mikutano ya hadhara ya siasa, na pia kupitia mikutano ya ndani ambayo inafanyika, ambapo baadhi ya wanasiasa wahuni wanamtukana Mheshimiwa Rais ambaye ndio kiongozi mkuu wa nchi, mimi sitakubaliana na hilo,” alisema Lugola.
Lugola amewataka wapinzani kuwa wasikivu kwa kufuata sheria za nchi na pia kutambua kuwa, Rais wa nchi hii ambaye kipenzi cha wananchi anapewa heshima yake kwa kuiletea maendeleo nchi.
Lugola alisema Rais Magufuli ni kiongozi ambaye kwa muda mfupi ameiletea mabadiliko makubwa nchi, na pia mipango mikubwa ya maendeleo inakuja katika uongozi wake.
Lugola alifanya mikutano miwili ya hadhara wilayani Kilosa, ambapo mkutano mmoja ulifanyika mjini Kilosa na mwingine ulifanyika Tarafa ya Kimamba wilayani humo, ambapo alizungumza na wananchi pamoja na kutatua migogoro ya ardhi wilayani humo kupitia kutoa nafasi kwa wananchi kutoa kero zao.
Aidha, Lugola aliwataka polisi nchini kuwa makini kwa kutenda haki wakati wanaletewa kesi za ardhi zenye jinai hasa katika Mkoa wa Morogoro ambao unakabiliwa na migogoro ya aina hiyo.
“Nimepata malalamiko ya baadhi ya polisi hapa Kilosa kutokutenda haki katika ukamataji wa watuhumiwa, polisi amepewa taarifa ya mtuhumiwa lakini hamkamati, sasa polisi ambaye ametajwa hapa mkutanoni hakumkamata mtuhumiwa huku uthibitisho ukionyesha kabisa mtuhumiwa amekosa na anapaswa kuwepo kituoni, naagiza polisi huyo akamatwe awekwe mahabusu,” alisema Lugola.
Pia aliwataka wananchi kutoa taarifa za wahamiaji haramu katika mkoa huo ili Uhamiaji iweze kuwakamata na kuwafungulia kesi wahamiaji hao kutokana mataifa mbalimbali wanaoingia nchini bila kufuata taratibu za nchi.
“Wakazi wa Kilosa, endeleeni kuchapa kazi, moto wa Magufuli mnauona, sasa hakuna uonevu, hakuna kauli ‘unanijua mimi nani’, nchi imetulia, maendeleo ya kasi mnayaona, huyu Magufuli hakika ameletwa na Mungu,” alisema Lugola.
Lugola amemaliza ziara yake ya siku tatu mkoani humo akitembelea Wilaya za Morogoro, Mvomero na Kilosa, akisikiliza kero za wananchi pamoja na kufuatilia maagizo yake aliyoyatoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo ndani ya Wizara yake.
Lugola mwaka jana mara alipoteuliwa kuiongoza Wizara hiyo, alitoa maagizo mbalimbali kwa Makamanda wa Polisi Mikoa nchini ambayo ni dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya polisi nchini, na pia kupiga marufuku tabia ya baadhi ya Polisi kubambikizia kesi wananchi, na pamoja na agizo la pikipiki zote zilizopo vituoni ziondolewe.