Siku chache baada ya kutoka mahabusu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amekumbana na pigo lingine baada ya uongozi wa Wilaya ya Hai kutangaza nia ya kupoka kiwanja chake.
Jana, uongozi wa wilaya hiyo ulitangaza kuwa tayari umeshawasilisha kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ilani ya ubatilisho wa umiliki wa wamiliki 34 wa viwanja vilivyoko eneo la maendelezo ya viwanda la Weruweru wilayani Hai.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, alidai wameamua kuchukua hatua hiyo kutokana na wamiliki wa viwanja hivyo kudaiwa kodi ya pango la ardhi.
Kwa mujibu wa Ole Sabaya, wamiliki hao wa viwanja 34, kwa pamoja wanadaiwa kodi ya pango la ardhi inayofikia Sh. 1,828,166,096.
Mbali na Mbowe, orodha ya wadaiwa hao iliyotolewa Ole Sabaya jana, pia ina majina ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Cynthia Ngoye, Kiwanda cha Kutengeneza Vipuri cha Kilimanjaro Mashine Tools Manufacturing Company Ltd kilichoko chini ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na wafanyabiashara maarufu wa Mji wa Moshi wanaomiliki shule binafsi na kampuni za utalii.
Akitangaza orodha hiyo jana, wakati wa mkutano wa siku mbili wa kusikiliza kero, malalamiko na migogoro ya ardhi wilayani mwake, Ole Sabaya alisema watu hao wamo kwenye orodha ndefu ya wamiliki ambao viwanja vyao vimeombewa kibali cha kufutwa.
Kwa mujibu wa Ole Sabaya, Kiwanda cha Mashine Tools kina deni la Sh. milioni 315.721 ambalo kinadaiwa kati ya mwaka 2010 na 2018.
“Huko nyuma, watu walipewa viwanja 52 vikubwa, wakaambiwa waendeleze kwa sababu ni eneo la viwanda, wana miaka mingapi? Ofisa Ardhi yuko wapi? Njoo, nini kimetokea pale?" Ole Sabaya alihoji.
“Sasa sikilizeni huo muziki, unapewa shamba (eneo la kiwanja) mwaka 1984, mmesikia? Kabla mimi sijazaliwa, hajawahi kufanya lolote, akapewa na halmashauri ili waendeleze kujenga viwanda.
"Sasa Ofisa Ardhi ameshaandika barua ya kubatilisha hivyo viwanja. Niwaambie hapahapa, wako watu mnaowaheshimu na hawalipi kodi na leo nitawataja humu.”
Katika mkutano huo, Ole Sabaya alipokea malalamiko 266 yanayohusu ardhi na kuahidi kuwa ndani ya siku mbili, yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi.
Kabla ya kutaja majina ya wadaiwa hao, Ofisa Ardhi Mteule Wilaya ya Hai, Jacob Muhumba, alisema: "Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, wengi waliopewa vile viwanja, wengine walipewa tangu mwaka 1984, wengine mwaka 2001, wa mwisho kabisa ni mwaka 2004. Wengi hawajaendeleza, lakini pia hawalipi kodi ya ardhi."
Kwenye orodha hiyo ya wadaiwa wa pango la ardhi ambayo imedaiwa kutumwa kwa Waziri Lukuvi, jina la Mbowe ni la 17 akidaiwa kumiliki kiwanja/shamba Na. 51.
Inadaiwa kuwa kiongozi huyo wa kisiasa ana deni la Sh. milioni 28.284 ambalo hajalilipa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2016 hadi 2018, wakati Hilda Ngoye anadaiwa Sh. milioni 18.688.
Majanga Yazidi Kumwandama Mbowe.....DC Lengai Ole Sabaya Ampokonya Kiwanja Chake
0
March 14, 2019
Tags