Makamu wa Rais Awapongeza Wakulima Shinyanga

Makamu wa Rais Awapongeza Wakulima Shinyanga
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amewapongeza wakulima wa mkoa wa Shinyanga kwa kuzalisha mazao ya biashara na chakula  kwa wingi na kufanya mkoa kuwa na chakula cha akiba kulinganisha na mikoa mingine.

Samia aliyabainisha hayo jana wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wilayani Kahama na kuelezea kufurahishwa kuona wakulima wengi mkoani Shinyanga wamejitokeza na kulima kwa wingi mazao ya chakula na biashara.

 Alisema mkoa wa Shinyanga kwa msimu wa kilimo uliopita, ulizalisha mazao ya biashara na chakula zaidi ya tani 500,000 na kuufanya kuwa na akiba ya chakula kingi cha kutosha.

Makamu wa Rais aliwataka wakulima mkoani hapa kuendelea kulima kwa wingi na kuuza mazao yao katika nchi za jirani na kuongeza kilimo kimekuwa kikiwanufaisha wakulima wengi na kimekuwa kikiingizia nchi fedha nyingi za kigeni.

Mbali na uzalishaji huo, aliwataka kukata bima za afya kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) iliyoboreshwa pindi wanapouza mazao yao na kupata fedha. Alisema hali hiyo itawafanya kumudu gharama za matibabu na kusababisha hospitali kuwa na dawa za kutosha, kwa kuwa fedha za bima ya afya zinatumika kununuliwa dawa na vifaa tiba.

  Alisema kuwa, Wilaya ya Kahama ina zaidi ya kaya 49,437 kati ya hizo ni 9,000 pekee ndizo zilizokata bima ya afya ya CHF, huku kundi kubwa likibaki likitumia gharama kubwa za matibabu.

 "Ndugu zangu wakulima, kateni bima za afya ili kumudu gharama za matibabu pindi mnapofika hospitalini kupatiwa huduma. Kumbukeni mnakunywa bia ngapi? Ni kiasi gani cha fedha mnapeleka nyumba ndogo na kwa nini mnashindwa kukata bima za afya? Alihoji Samia.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Inocent Bashungwa, alisema kutokana na mkoa wa Shinyanga kulima mazao mengi ya kibiashara, serikali ina mkakati wa kujenga kiwanda kikubwa  cha usindikaji wa mazao Kanda ya Ziwa ili nchi za jirani za Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrassi ya Congo zifike Kahama kununua mazao.

Alisema serikali imekuwa ikiwajali wakulima kwa kuwapelekea pembejeo kwa muda mwafaka ikiwa ni pamoja na kuwatafutia masoko ya kuuza mazao yao na kwamba kila mkulima ana wajibu wa kuuza mazao yake katika nchi za jirani ili kujiongezea kipato.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad