Mama Samia Aelekea Uganda Kumwakilisha Rais Magufuli Kwenye Mkutano wa Africa
0
March 11, 2019
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anaondoka nchini leo kuelekea Kampala, Uganda kushiriki kwenye Mkutano wa mwaka 2019 wa ‘Africa Now Summit’unaotarajiwa kufanyika tarehe12 na 13 Machi.
Mkutano huo utafunguliwa na Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni ambaye ndiye Mwenyeji wa mkutano huu. Mkutano utakuwa na mada mbalimbali ikiwemo ya Uongozi unaohitajika kuchochea mabadiliko ya Kijamii na Uchumi Afrika, mada hii itatolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Viongozi wengine watakaotoa mada ni Rais wa Misri ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (UA) Mhe. Abdel Fattah el Sisi; Rais wa Afrika Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa; Makamu wa Rais wa Kenya Mhe. William Ruto; na Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Ahmed Abiy. Mada zote hizi zitajikita kwenye kuonesha chachu ya Uongozi katika kuleta maendeleo endelevu barani Afrika.
Mkutano utamalizika tarehe 13 Machi 2019 utaanza na hotuba kutoka kwa Rais wa Somalia Mhe. Mohamed Abdullahi na baadae kufungwa rasmi na mwenyeji wake Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni.
Makamu wa Rais ataambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro.
Tags