HATIMAYE klabu ya Manchester United imemchukua rasmi Ole Gunnar Solskjaer kuwa kocha na kumpa mkataba wa miaka mitatu baada ya kung’ara katika kipindi alichofanya kazi kama kocha wa muda.
Kocha huyo raia wa Norway alifufua nguvu za klabu hiyo tangu akabidhiwe timu baada ya kutimuliwa kwa Mreno Jose Mourinho mwezi Desemba mwaka jana. Tangu hapo ameshinda mechi 14 kati ya 19 na kuwaongoza Mashetani Wekundu hao kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
Solskjaer, ambaye alifunga mabao 126 katika mechi 366 alizoichezea United, na alishakuwa shujaa kwa mashabiki wa klabu hiyo ya soka, alijipatia sifa ya kuwa mtu aliyefunga bao katika muda wa majeruhi wa fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya mwaka 1999 na kuiwezesha timu hiyo kutwaa vikombe vitatu katika msimu mmoja.
“Kutoka siku ya kwanza niliyowasili, nilijisikia kama niko nyumbani katika klabu hii ya aina yake,” Solskjaer alisema katika taarifa yake iliyowekwa kwenye tovuti ya klabu hiyo.
“Ni heshima kuwa mchezaji wa Manchester United na baadaye kuanzia kazi ya ukocha hapa.
“Miezi michache (niliyofundisha hapa) imekuwa ya aina yake na nataka kuwashukuru makocha wote, wachezaji na wafanyakazi kwa kazi ambayo tumeshaifanya hapa hadi sasa.
“Hii ni kazi ambayo wakati wote nimekuwa nikiota kuifanya na nimefurahi kupita kiasi kupata nafasi ya kuongoza klabu kwa kipindi kirefu na natumaini tutaendelea kuleta mafanikio ambayo mashabiki wetu wanayataka,” alisema.
Makamu mwenyekiti mtendaji wa United, Ed Woodward alisema: “Mbali ya kiwango na matokeo, Ole analeta uzoefu mkubwa, kama kocha na mchezaji, ukijumlishwa na nia ya kuwapa wachezaji vijana nafasi na ufahamu mkubwa wa utamaduni wa klabu.”
Man U Yampa Rasmi Ole Gunnar Solskjaer Mkataba wa Miaka 3
0
March 28, 2019
Tags