Marekani yatoa zawadi ya mabilioni kwa Atakayefanikisha Kumkamata Mtoto wa Osama Bin Laden


Marekani imetangaza zawadi ya $1 milioni (sawa na 2,345,300,000 za Tanzania) kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa mtoto wa kiume wa kiongozi wa Al-Qaeda, Osama Bin Laden.

Taarifa rasmi ya Serikali ya Marekani imeeleza kuwa Hamza Bin Laden amekabidhiwa jukumu la kuwa kiongozi wa Al-Qaeda na anapanga mashambulizi ya kigaidi.

“Serikali ya Marekani inatoa zawadi kwa taarifa kuhusu Hamza Bin Laden. Tunawahakikishia usiri mkubwa na uwezekano wa kuhamishwa eneo ulipo upo. Kama unazo taarifa, tafadhali wasiliana na ubalozi wa Marekani ulio karibu nawe,” tafsiri ya sehemu ya taarifa ya Marekani.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa Hamza anaweza kuwa karibu na mipaka ya Afghanstan na Pakistani.

Hivi karibuni, alisambaza video na sauti zenye jumbe za kuwahamasisha wafuasi wa kundi hilo duniani kutekeleza mashambulizi dhidi ya Marekani na marafiki wao wa Magharibi kwa lengo la kulipiza kisasi cha kifo cha baba yake.

Mwaka 2011, kikosi namba mbili cha makomando wa Marekani kilivamia maficho ya Osama Bin Laden katika mji wa Abbottabad nchini Pakistani na kumuua. Osama anatajwa kuagiza utekelezaji wa mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001 nchini Marekani ambayo yalisababisha vifo vya takribani watu 3,000.

Hamza Bin Laden ambaye anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 hivi sasa, anadaiwa kuwa amemuoa binti wa Mohammed Atta, ambaye alihusika kuteka moja kati ya ndege za abiria na kugonga mnara wa jengo la Biashara (World Trade Center) jijini New York.

Barua ambazo zilipatikana kwenye nyumba ya Osama baada ya kuuawa, zinadaiwa kuonesha jinsi ambavyo alikuwa akimkubali na kumpa nafasi Hamza kama mtoto wake mpendwa zaidi na ambaye anaweza kuchukua jukumu la kuiongoza Al-Qaeda.

Osama ambaye ni mzaliwa wa Saudi Arabia alienda Afghanistan miaka ya 1980 ambapo alijiunga na kundi la Mujahideen lililokuwa linasaidiwa na Marekani kupigana na vikosi vya Soviet ambavyo vilikuwa vimeikalia ardhi ya Afghanistan.

Alianzisha taasisi kwa kwa ajili ya kuwasaidia watu waliokuwa wanajitolewa kuungana na Mujahideen kupigana kuikomboa ardhi ya Afghanistan, aliita taasisi hiyo ‘Al-Qaeda’. Mwaka 1989 aliondoka Afghanistan. Alirejea tena mwaka 1996 na kuanzisha kambi ya kutoa mafunzo ya kijeshi kwa maelfu ya wapiganaji wenye mlengo wa imani ya itikadi kali.

Baada ya muda, Al-Qaeda ilitangaza rasmi vita dhidi ya Marekani, Israel na washirika wao.a

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad