Marekani yawawekea vikwazo maafisa wa tume ya uchaguzi DR Congo

Marekani yawawekea vikwazo maafisa wa tume ya uchaguzi DR Congo
Serikali ya Marekani imewawekea vikwazo maafisa watatu wa tume ya uchaguzi nchini DR Congo pamoja na wale wa serikali ya aliyekuwa rais wa taifa hilo Joseph kabila kwa tuhuma za ufisadi.

Taarifa iliochapishwa katika mtandao wa wizara ya fedha nchini Marekani, inasema kuwa watatu hao walidaiwa kula rushwa ili kuzuia na kuchelewesha maandalizi ya uchaguzi wa haki na ulioshirikisha pande zote.

Watatu hao ni rais wa tume ya uchaguzi nchini DRC Corneille Yobeluo Nangaa (Nangaa), naibu wake Norbert Basengezi Katintima (Katintima), na mwanawe Katintima, Marcellin Basengezi Mukolo (Basengezi), ambaye ni mshauri mkuu katika tume hiyo ya uchaguzi CENI.


Kulingana na taarifa hiyo iliotiwa saini na katibu wa maswala ya ugaidi na intelijensia ya kifedha nchini Marekani Sigal Mandelker, watuhumiwa hao walifanya vitendo ambavyo vilikandamiza mikakati ya kidemokrasia au taasisi zake nchini DRC.

''Hii leo idara ya fedha inayosimamia mali ya kigeni OFAC imewawekea vikwazo maafisa watatu wakuu wa tume ya uchaguzi nchini DR Congo CENI kwa kukandamiza demokrasia nchini DRC'', ilisema taarifa hiyo.

Matokeo ya Uchaguzi huo uliompatia ushindi rais aliyeko madarakani Felix Tshisekedi ulipingwa na jamii ya kimataifa ikiwemo Marekani pamoja na mpinzani mkuu wa Joseph kabila katika uchaguzi huo Martin fayulu.

Matokeo yaliyotangazwa na CENI:
Felix Tshisekedi 7,051,013 (38.57%)
Martin Fayulu Madidi 6,366,732 (34.83%)
Emmanuel Shadary 4,357,359 (23.84%)
*Waliojitokeza kupiga kura kwa mujibu wa CENI ni 47.56%.

Katika taarifa hiyo Marekani imesema kuwa inaunga mkono hatua ya raia wa DR Congo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi huo wa Disemba 30 licha ya kuwa bado ina wasiwasi kuhusu mchakato mzima wa uchaguzi huo ambapo inaishutumu tume ya uchaguzi nchini humo CENI kwa kushindwa kuhakikisha kuwa matokeo ya kura hiyo ni sambamba na matakwa ya raia hao.

Imesema kuwa Marekani itaendelea kuwasaidia wale walio tayari kukabiliana na ufisadi lakini haitasita kuwachukulia hatua kali wahusika wanaokandamiza mchakato wa kidemokrasia na kuendeleza ufisadi nchini DRC na ulimwenguni kwa jumla.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad