Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati akitoa tathmini ya hali ilivyo katika magereza nchini baada ya kukaa huko zaidi ya miezi mitatu amesema kuwa magereza kuna ugonjwa wa ngozi ambao chanzo chake ni kunguni na chawa ambao chanzo chake ni uchafu uliokithiri.
"Ugonjwa huu wanauita burudani kwa sababu mtu ukilala unajikuna sana mwisho wa siku unaathiri viungo vya mwili mtu anaweza kukaa wiki hajaoga na wanalala godoro futi tatu wanalala wanne, mmoja akiupata ugonjwa hapo ni wote, ugonjwa huu unawatesa sana wafungwa," amesema Mbowe.
Mbowe amewaomba jaji mkuu, jeshi la polisi pamoja na kamishna wa magereza kufanya operesheni ya safisha magereza kwa sababu mkakati huo utasaidia kuondoa nusu ya maabusu wanaongezeka magerezani kutokana na upelelezi na uchunguzi wa kesi zao kutokamilika kwa wakati.
"Maabusu wakifikishwa wanaambiwa upelelezi unaendelea, watu hawa wanalalamika, wanafutiwa mashtaka na kufunguliwa mashtaka, katika operesheni hii ya magereza hawa watu waangaliwe, kama kweli wanahusika na ugaidi wanapelekwa mahakamani kwa ulinzi mkali, basi wahukumiwe, tunawafanya hawa watu wawe magaidi zaidi na wanafundishwa wawe raia wasiojua kuheshimu sheria," amesema Mbowe.
Aidha Mbowe ameviomba vyombo husika kutafakari kuhusu suala hilo kwa sababu wakifanya hivyo watatambua nusu yao hawana kesi. Mbowe ameomba mahakama za mwanzo zimulikwe sana kwa sababu watu hawapati haki zao kwa wakati.