Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema kilichotokea kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuhamia Chama cha ACT- Wazalendo ni sehemu ya mapambano.
Mbowe amesema hayo leo Jumatatu Machi 18 ikiwa ni muda mfupi kupita tangu Maalim Seif autangazie umma wa Watanzania kuwa yeye, viongozi na wanachama wa chama hicho wanaomuunga mkono wanahamia ACT- Wazalendo.
“Maalim na timu yake bado ni sehemu muhimu sana katika mapambano haya, tunawatakia kila la kheri,” amesema Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania.
Licha ya kuwatakia maisha mema huko ACT- Wazalendo lakini amewaomba wakafanye siasa kuanzia ngazi za chini ili kuhakikisha malengo ya kuwapigania wananchi yanafikiwa.