Mchungaji Mashimo Matatani Kisa Kifo cha Kibonde
0
March 20, 2019
MCHUNGAJI wa Kanisa la Emmaus Bible Church, Mbezi Luis jijini Dar, Daudi Mashimo amejikuta mikononi mwa polisi baada ya kuzungumzia kifo cha mtangazaji wa Clouds FM, Ephraim Kibonde, Ijumaa Wikienda lina habari kamili.
NI IJUMAA ILIYOPITA
Kwa mujibu wa chanzo chetu makini, mchungaji huyo alijikuta matatani Ijumaa iliyopita katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay ambapo alishikiliwa kuanzia majira ya saa 5 asubuhi mpaka jioni alipoachiwa. “Aliwekwa pale kituoni kuanzia mida kama ya saa tano hivi wakamuachia jioni sana baada ya kumuweka kitimoto cha maswali yao kuhusu Kibonde,” kilidai chanzo hicho.
KILICHOMPONZA
Mara baada ya kifo cha Kibonde kutokea Machi 7, mwaka huu, mchungaji Mashimo aliibuka na kutoa kauli kwamba mtangazaji huyo hajafa jambo ambalo liliwashangaza wengi ambao wanaamini kifo kikishatokea, kimetokea. “Kilichomponza ndio hicho, ameonekana kama anataka kusababisha vurugu kwa familia ambayo inaamini mpendwa wao ameshafariki,” kilieleza chanzo makini.
AANDAA PRESS
Kuonesha kwamba amedhamiria kuzungumzia kinaga ubaga jambo hilo la Kibonde, mchungaji Mashimo aliona awatumie jumbe wanahabari kuonesha dhamira yake ya kufanya mkutano wa waandishi (press) ili aweze kufafanua kiundani. Press hiyo alipanga kuifanya Ijumaa iliyopita lakini badala yake, alitakiwa ajisalimishe kituo cha polisi kwa ajili ya mahojiano.
“Siku hiyohiyo ambayo ilikuwa afanye press, polisi walimuita ambapo walikaa naye kuanzia asubuhi mpaka jioni, kikubwa walikuwa wanamhoji na kumuelekeza aache kuleta uchonganishi kutokana na kauli yake aliyoitoa kuhusu Kibonde kuwa yupo hai,” kilimalizia chanzo hicho makini.
HUYU HAPA MASHIMO
Baada ya kupewa ubuyu huo, Ijumaa Wikienda lilimtafuta mchungaji Mashimo, Ijumaa iliyopita kupitia simu yake ya mkononi ambapo alipopatikana alithibitisha kushikiliwa na polisi na kueleza msimamo wake kuhusu suala hilo la Kibonde. “Unajua watu wanashindwa tu kunielewa kwamba si mimi bali ni Mungu mwenyewe anasema kupitia mimi. Nimeshaoneshwa mambo mengi huko nyuma nikayasema na kweli yakadhihirika mbona watu walikuwa hawashangai.
“Kwa hili la kifo nasimamia msimamo wangu, yaani mpaka kesho huo ndio unabii wangu, mimi ni mtumishi wa Mungu nini kosa langu…ni maono hata kama wamenipiga marufuku siwezi kuacha kutoa unabii, nitaendelea kumsikiliza Mungu tu, haya ndio maisha yangu hivyo siwezi kuacha kuongea kile ambacho Mungu amenionesha,” alisema mchungaji.
KAMANDA KINONDONI AFUNGUKA
Ijumaa Wikienda lilizungumza na Kamanda wa Kinondoni, Mussa Athumani Taibu ambaye alithibitisha kumhoji mchungaji Mashimo kwa saa kadhaa kabla ya kumuachia. “Tulimwita kwa shida zetu akidaiwa kusema kuwa Kibonde hajafa, wamezika mgomba anaweza kuleta uchonganishi kwa familia ikapelekea ramli chonganishi ambayo huleta maafa, hatujamzuia kufanya mikutano wala kuhubiri neno au mafundisho ya Mungu. Hicho tu ndicho tulichomwitia,” alisema kamanda Musa.
Kibonde alifariki baada ya kuugua ghafla mjini Bukoba alipokwenda kumzika aliyekuwa bosi wake, Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group (CMG), Ruge Mutahaba na kuzikwa Machi 9, mwaka huu katika Makaburi ya Kinondoni jijini Dar.
Stori: GPL
Tags