Mgombea uenyekiti wa Taifa katika Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Profesa Ibrahim Lipumba, Diana Simba, amesema si kwamba Lipumba ndiye msomi pekee kwani hata yeye ana Stashahada ya Maendeleo ya Jamii hivyo anaamini anaweza kukiongoza chama hicho.
Diana ambaye ni mwanamke pekee anayegombea nafasi hiyo amejikuta katika wakati mgumu wakati wa kujinadi na kuomba kura kutokana na aina ya maswali aliyokuwa akiulizwa.
Elimu, uzoefu ndani ya chama na nchi alizowahi kutembelea ni kati ya maswali yaliyoelekezwa kwa mgombea huyo na alipokuwa akijibu baadhi ya wajumbe walisikika wakimkejeli hatua iliyosababisha msimamizi kuchukua kipaza sauti mara kwa mara kuwasihi watulie wamsikilize mgombea.
“Nilijiunga na chama mwaka 2017 na nimetembelea Kenya na Uganda, msifikiri Profesa Lipumba ndiye msomi peke yake hata mimi ni msomi. Nina Diploma ya Maendeleo ya Jamii hivyo nina uwezo wa kuwaongoza,” amesema Diana.
Awali, akizungumza kwenye mkutano huo leo Jumatano Machi 13, 2019 Profesa Lipumba alisema kwa sababu ni miongoni mwa wagombea wa nafasi ya uenyekiti hawezi kuwa mwenyekiti wa kikao hicho.
Alisema kwa mujibu wa katiba, kanuni na taratibu za chama hicho kikao kipendekeze mwenyekiti wa muda.
Aliwauliza wanachama kwa ujumla wao wanamtaka nani awe mwenyekiti wa muda wakajibu. ‘Milambo Yusuph Kamili’ hivyo akamtangaza kuwa ndiyo mwenyekiti wa muda wa kikao hicho.
Lipumba alitoa ufafanuzi wa uchaguzi utakavyofanyika kuwa wataanza na kumchagua mwenyekiti wa taifa, akifuatia makamu mwenyekiti Zanzibar na kumalizia na makamu mwenyekiti Tanzania Bara.
Pamoja na Profesa Lipumba wengine kwenye kinyang’anyiro hicho ni Diana Daudi Simba na Zuberi Mwinyi Hamisi. Mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe 798.
Mgombea Uenyekiti CUF Ajifananisha na Lipumba Akiomba Kura
0
March 13, 2019
Tags