Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mh. Joachim Wangabo amelazimika kuacha gari lake na kutembea kwa mguu ili kukifikia moja ya kijiji kilichopo Wilaya ya Kalambo mkoani humo kutokana na miundombinu mibovu ya barabara.
Hali hiyo imetokea wakati alipokuwa katika ziara ya kutembelea kijiji cha Nondo, Kata ya Mpombwe Wilaya ya Kalambo kwaajili ya kukutana na wananchi hao na kufahamu changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo.
Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na wataalamu kutoka katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Msafara huo ulikwama kwenye tope zito lililosababishwa na mvua zilizonyesha hivi karibuni na kusababisha hali ya barabara kuwa mbaya.
Hali hiyo ilipelekea Mkuu wa Mkoa na msafara wake kutembea kwa mguu kwa takribani saa moja na nusu kufika katika kijiji hicho, ambapo walivuka madaraja mbalimbali ya miti ambayo yana usalama mdogo kwa wananchi wa vijiji vinavyotumia barabara hiyo.