Wafanyabiashara wanahesabu hasara baada ya mali ya thamani isiyojulikana kuteketea Jummane alfajiri katika soko la Toi mjini Nairobi
Moto umewaka mwendo wa saa tisa Jumanne alfajiri katika soko la Toi mjini Nairobi.
Ni soko maarufu linalofahamika kwa uuzaji wa bidhaa kukuu zikiwemo nguo za mtumba, lakini pia bidhaa nyingine kama mbao na vifaa vya elektroniki.
Muuzaji mmoja Charlie Chaplin ameiarifu BBC kwamba aliamshwa alfajiri kwa simu akiarifiwa kwamba moto umezuka na alilazimika kukimbia kwenda katika soko hilo. Kwa sasa anasema anakadiria hasara ya mamilioni ya shilingi za Kenya.
Mwandishi habari aliyefika katika eneo hilo Oliver Koech, anasema baadhi wamelalamika kuhusu kujivuta kwa idara za zima zoto kukabiliana na moto huo kwa wakati mzuri na kuudhibiti kabla ya kusambaa kama ulivyosambaa na kuiharibu sehemu kubwa ya soko hilo. Sio mara ya kwanza magari ya zima moto kushutumiwa nchini kwa kushindwa kudhibiti mikasa ya moto kwa muda muafaka na licha ya kuwa na vifaa vipya.
Makazi yasiyo rasmi kama vijiji yanakuwa hayana mpangilio mzuri, nyumba husongamana sana na hakuna njia za katikati, hivyo magari ya zima moto hushindwa kuingia ndani zaidi. Kufikia saa moja asubuhi ya leo, baadhi ya wauzaji walikuwa wakijaribu kukusanya masalio ya mali zao katika eneo hilo la Toi.
Wauzaji wengi wanahesabu hasara ya thamani ya mali isiyojulikana katika soko hilo lililo karibu na mtaa mkubwa wa mabanda Kibera mjini Nairobi.
Wanasema ni pigo kubwa, na hawajui la kufanya kutokana na kwamba walitegemea biashara katika soko hilo kujikumu maisha.
Moto Wateketeza Mali ya Thamani Isiyojulikana Nairobi
0
March 12, 2019
Tags