KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera amewahakikishia mashabiki wa Yanga kwamba amezungumza na Yusuf Manji uso kwa uso kwa mara nne na uwezekano wa kurejea Jangwani ni mkubwa.
Zahera ambaye ni Kocha wa Yanga mwenye uraia wa DR Congo na Ufaransa, amekiri kwamba Mwenyekiti huyo wa zamani wa Yanga ni miongoni mwa viongozi wachache wenye akili sana na anajua mambo.
Kocha huyo mwenye Diploma ya Ukocha ya Uefa aliyoipata Ufaransa, amesema wakati akipiga stori na Manji alikuwa na Viongozi wengine wa Yanga Jijini Dar es Salaam hivik aribuni. “Nimezungumza na Manji kama mara nne tofauti, tumekutana kwenye vikao tofauti nikiwa pamoja na viongozi wengine wa Yanga.
“Tumezungumza mambo mengi sana kuhusiana na Yanga na amezungumza na sisi kwa uwazi kabisa, ila nlichokiona anasubiri kwanza hali ikae sawa,”alisema Zahera alipofanya ziara juzi Jumanne kwenye ofisi za Spoti Xtra zilizopo Sinza Mori Jijini Dar es Salaam.
“Inaonekana kuna sehemu ndani ya Yanga kuna baadhi ya vitu ambavyo vinakwenda kwenye hali fulani ambayo haimpendezi sana ndiyo maana hajaweka fedha yake kwenye uendeshaji. Maana unajua yule ni mfanyabiashara hawezi kuweka fedha tu bila kuwa na mamlaka nazo.
“Unajua mimi nikikaa na wewe dakika tano naweza kujua una akili au huna. Ila baada ya kikao cha Manji niliwaambia wale viongozi kwamba huyu jamaa anajua, ana akili sana.
“Ukimsikiliza mipangilio yake na kile anachokisema ni ukweli kabisa na ni vitu ambavyo vinatekelezekana na vinaweza kuifanya Yanga ikapiga hatua. “Kwa jinsi nilivyomsikiliza na kumuelewa Manji atarudi Yanga, atarudi tu ni suala la muda tu,” alisema Zahera na kusisitiza kwamba Manji anaona huruma sana mambo yanavyokwenda sasa ndani ya Yanga.