Wakati watu mbalimbali wakitarajia kumuona aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari akijitokeza kueleza kiundani ni kipi ambacho kilitokea juu ya sakata lake la kuvuliwa Ubunge Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na yeye amemtaka kufanya hivyo.
Mbowe ametoa kauli hiyo katika Mkutano wake wa jana na waandishi wa habari uliofanyika jana Jijini Dar es salaam, ambapo hakutaka kueleza kiundani bali alieleza suala hilo limekaa kiutawala zaidi na amemtaka Nassari mwenyewe afunguke ukweli wa suala hilo.
Kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii Nassari mwenyewe aliandika ujumbe ulioashiria kuwa leo ataweka wazi juu ya ukweli wa suala hilo.
"Watanzania, watu wangu wa Meru tumefanyiwa dhuruma na uonevu, nitazungumza kesho (leo Jumamosi Machi 16, 2019) na vyombo vya habari undani kuhusu jambo hili".
Lakini juu ya sakata hilo pia limeonekana kumfurahisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, ambaye na yeye aliandika ujumbe wa kumpongeza Nassari kwa kile alichokiandika kuwa amefanya maamuzi sahihi.
"Kaka nakupongeza sana kwa busara uliyotumia kuwa sehemu ya ukweli, sisi ni vijana, tuendelee kishirikiana tuko pamoja" aliandika Gambo kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Mapema wiki hii Spika wa Bunge Job Ndugai, alitangaza kumvua Nassari ubunge wa jimbo la Arumeru Mashariki kwa makosa ya mahudhurio hafifu bungeni ikiwemo kukosa vikao vya mikutano mitatu ya bunge.