Shughuli mbalimbali ikiwemo shule na ofisi za serikali nchini Venezuela, zimesitishwa kwa saa 48 kuanzia jana Machi 11, 2019, kutokana na kukosekana kwa umeme nchi nzima tangu alhamisi mchana Machi 7, 2019.
Rais wa nchi hiyo ya Amerika ya Kusini, Nicolas Maduro ameishutumu Marekani kuwa ndio walioshambulia miundombinu ya umeme, japo amekiri kuwa hawajathibitisha hilo bado.
Kwa mujibu wa kiongozi wa upinzani nchini humo Juan Guaido, mpaka sasa ikiwa inakaribia siku ya 5, baadhi ya maeneo muhimu hayana umeme ikiwemo hospitali na watu takribani 17 wamepoteza maisha kwa kushindwa kufanyiwa upasuaji.
Imeelezwa kuwa hitilafu kubwa imetokea katika mitambo mikuu ya kuzalisha umeme katika mji mkuu wa Venezuela Caracas hivyo kusababisha kukosekana kwa umeme katika eneo kubwa la nchi.
Maduro ameendelea kusisitiza kuwa umeme utarejea taratibu katika maeneo ya Caracas na kwingine huku akiweka wazi kuwa huo ni mpango wa upinzani kumwondoa madarakani kwa kushirikiana na nchi za Marekani na Ulaya.