Baada ya kukamilisha dili la kujiunga na klabu ya MFK Vyskov ya daraja la pili Jamhuri ya Czech, nyota aliyetokea chimbuko la Serengeti Boys, Ally Ng'anzi amejiunga na klabu ya Minnesota United ya nchini Marekani.
Ng'anzi mwenye umri wa miaka 18 amejiunga na Minnesota United inayoshiriki ligi kuu ya nchini Marekani kwa mkopo wa mwaka mmoja baada ya kukamilisha vipimo vya afya na klabu hiyo mapema jana Jumatatu.
Katika moja ya vipengele vya mkataba huo wa mkopo, ni kuwa mchezaji huyo anaweza kununuliwa moja kwa moja endapo atafanya makubwa kwenye klabu hiyo yenye maskani yake Minneapolis, state.
"Kucheza Marekani hasa MLS ni ndoto yangu ukubwa na Ligi yao na ile niliyokuwa nikicheza ni tofauti najivunia kwenda kucheza na mastaa makubwa ambao walitamba kwenye soka la Ulaya", amesema Ng'anzi.
Pia kwa mujibu wa taarifa kutoka klabu ya Minnesota United, nyota huyo atapelekwa kwa mkopo katika klabu ya Forward Madison inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini humo kwa mwaka huu 2019.