Papa Francis: Kuzuia Watu Kubusu Pete Yangu ni Suala la Kiafya na si Vinginevyo

Papa Francis: Kuzuia Watu Kubusu Pete Yangu ni Suala la Kiafya na si Vinginevyo
Papa Francis amevunja ukimya juu ya mkasa wa kuzuia waumini kubusu pete yake akisema lilikuwa ni suala la kiafya zaidi.

Msemaji wa Vatican Alessandro Gisotti amesema kuwa Papa alikuwa akihofia kusambaa kwa vijidudu alipokuwa waumini wa Kanisa Katoliki siku ya Jumatano.

Wahafidhina ndani ya kanisa walipinga vikali kitendo hicho wakidai Papa anavunja utamaduni wa muda mrefu wa kanisa.

"Lilikuwa tu ni suala la kiafya," Bwana Gisotti amesema siku ya Alhamisi, akiwaambia maripota kuwa yeye mwenyewe alimuuliza Papa juu ya suala hilo.


Gisotti amesema kuwa kulikuwa na watu wengi waliokuwa kwenye msururu wa kumsalimia Papa na yeye akawa na tahadhari juu ya uwezekano wa kusambaza vijidudu.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki mwenye miaka 82 anadaiwa kuwa "kufurahishwa" na utata huo, msaidizi wa Papa ameliambia shirika la habari la Reuters.

"Papa anapenda kuwakarimu watu, na yeye pia hupenda kukarimiwa", amesema Gisotti na kuongeza kuwa Papa hufurahia kuwaruhusu watu kwenye makundi madogo kubusu pete yake.

Mkanda mrefu zaidi wa tukio hilo unaonesha kuwa Papa aliwaruhusu watu wachache kuinama na kubusu pete yake.

Siku iliyofuata Papa alionekana akiwaruhusu watawa na makasisi kubusu pete yake katika barza yake kuu ya Mji wa Vatican huko Roma.

Papa 'ahofia' makasisi wapenzi wa jinsia moja
Changamoto kubwa inayomkabili Papa kwa sasa
Pete ya Papa, inayovaliwa kwenye kidole cha kati cha mkono wa kulia ndiyo alama yenye nguvu zaidi ya utawala wa Papa.

Kubusu pete hiyo - ni utamaduni ulioasisiwa miongo mingi iliyopita - inachukuliwa kama alama ya heshima na utii kwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki.

Mara tu baada ya Papa kufariki, pete yake mara moja huteketezwa ikiwa ni kiashiria kuwa utawala wake umefikia kikomo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad