Polisi wazuia mkutano CUF upande wa Lipumba ......, Wenyewe wagoma, Waendelea na mkutano

Mkutano Mkuu wa saba wa Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Profesa Ibrahim Lipumba, umeingia dosari baada ya Jeshi la Polisi kuingilia kati na kusema kuna zuio la mahakama.

Mkutano huo unaofanyika leo Jumanne Machi 12, Buguruni jirani na ofisi za chama hicho umeanza asubuhi kwa wajumbe kutoka maeneo mbalimbali nchini kuwasili na wakati zoezi la uhakiki likiendelea, polisi walifika na kuwataka kutoendelea na mkutano huo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Zuberi Chembera, ambaye aliongozana na maofisa kadhaa wa polisi alifika katika ukumbi unakofanyika mkutano huo na kuzungumza na viongozi wa chama hicho wakiwemo Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya na Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Abdul Kambaya na kuwataka kutoendelea na mkutano.

“Sisi tumeleta taarifa kwamba mkutano una zuio,” alisema Chembera.

Hata hivyo viongozi hao wa Cuf walisema wataendelea na mkutano kwa sababu hawajaona nakala ya maandishi ya zuio hilo.

“Mkutano hauna zuio, je kuna ‘document’ umekuja nayo kamanda….ungekuja nayo tungekuelewa, sisi tunaendelea na mkutano wetu,” alisikika mmoja wa viongozi wa Cuf.

Mkutano huo ambao waandishi wa habari hawaruhusiwi kuingia ukumbini umefunguliwa na Naibu Msajili, Sisty Nyahoza .

Katika hotuba yake, Nyahoza amesema mkutano huo unafanyika kwa mujibu wa Katiba ya CUF ndio maana umetambuliwa na Ofisi yake.

Amewapongeza kwa kile alichosema wamehimili mapito ya mahakama na wameendelea kukilinda chama.

Vilevile amewapongeza kwa kuteua bodi mpya ya wadhamini na kuwakumbusha wajibu wao wa kutunza Mali na fedha.

Amewataka pia kuzingatia mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa.

Nyahoza pia amesema sheria ya sasa ya vyama vya siasa hairuhusu vyama kuwa na vikundi vya ulinzi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad