Profesa Lipumba ashinda uenyekiti CUF kwa kishindo
0
March 14, 2019
Profesa Ibrahim Lipumba amechaguliwa kwa kishindo kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) ngazi ya Taifa kupitia uchaguzi uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Lipumba amechaguliwa kwa kura 516 ambazo ni sawa na asilimia 88 ya kura zote, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi huo, Thenei Ally. Hatua hiyo inampa mwanazuoni huyo nafasi nyingine ya miaka mitano ya kuwa Mwenyekiti wa CUF.
Aidha, Naftaha Nachuma alifanikiwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho akijipatia asilimia 40.9 ya kura zote zilizopigwa.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Profesa Lipumba amesema kuwa hivi sasa amejipanga katika kuhakikisha wanajenga chama hicho na kuondoa migogoro. Ameeleza kuwa migogoro iliyokitikisa chama hicho imekiimarisha zaidi baada ya kufanikiwa kuendelea kuwepo.
“Nashukuru kwa kunichagua tena, hii itakuwa awamu yangu ya tano. Tuna changamoto kubwa tumeingia katika mgogoro, lakini mimi nauhesabu ule mgogoro umekuwa kama vile chuma umekipitisha kwenye moto, na chuma ukikipitisha kwenye moto kikitoka salama kinakuwa chuma imara zaidi,” alisema Profesa Lipumba.
Alieleza kuwa katika awamu hii wataendelea kujenga uaminifu na msimamo wa chama wa haki sawa kwa wote ambao unawavutia watu wengi.
Profesa Lipumba ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, aliingia kwenye mgogoro mkubwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad katika harakati za uchaguzi mkuu na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Zari azua hofu na drip sita kitandani, asema shetani muongo
Mwanasiasa huyo aliwasilisha barua ya kujiuzulu uenyekiti wake akipinga kitendo cha Ukawa kumkaribisha Edward Lowassa kugombea urais, lakini baada ya uchaguzi alirejea na kuahirisha uamuzi wake katika kile alichokieleza kuwa barua yake bado haijajadiliwa.