RAIS John Magufuli ameonyesha kutoridhishwa na namna ambavyo suala la upelelezi wa tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ linavyofanya na Jeshi la Polisi nchini huku akidai sakata hilo linaacha maswali yasiyojibika kwa wananchi.
Magufuli amesema hayo leo Jumatatu, Machi 4, 2019 wakati akihutubia baada kuwaapisha Balozi Dk. Augustine Phillip Mahiga kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Prof. Palamagamba John Mwaluko Aidan Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
“Kazi ya kuteua Makamishna wa Jeshi la Polisi haikuwa ndogo, nilimuita Waziri wa Mambo ya Ndani na Katibu Mkuu wa Wizara. Huwezi kuwa Kamanda wa Oparesheni kisha askari wako wanauawa. Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri ukiacha kasoro ndogo
“Jeshi la Polisi linatakiwa kuelewa kuwa Watanzania sio wajinga, kama suala la kutekwa kwa Mo Dewji linaacha maswali. Tuliambiwa alitekwa na Wazungu, lakini alitelekezwa Gymkhana kwenye gari na bunduki zikaachwa pale. Unajiuliza huyu mtekaji aliondoka na bunduki akaziacha, je angekutana na polisi wakimtafuta? Wakajaribu kulichoma moto gari, lakini baadaye tunamuona aliyetekwa akinywa chai na Mambosasa, maelezo hayapo.
“Baada ya siku chache tukaambiwa nyumba aliyokuwa katekwa Mo Dewij hii hapa na dereva aliyekuwa anawabeba watekaji huyu hapa, tukahisi atapelekwa mahakamani akatoe maelezo, baadaye kimya mpaka leo miezi imepita, hakuna aliyepelekwa Mahakamani. Labda ndiyo mambo ya kisasa, hata mmiliki wa nyumba hakuhojiwa, ile inatoa maswali mengi ambayo hayana majibu. Hata kama Watanzania watanyamaza lakini mioyo yao haitakuwa ‘clear’.
“Mambo haya yanalitia doa Jeshi la Polisi. Lazima tujenge taswira ya Jeshi la Polisi kama lilivyoasisiwa na Mwalimu Nyerere. Kama kuna maofisa wa Jeshi la Polisi wanaofanya vibaya leta taarifa ili hata nyota zao zipunguzwe na wanaoshindwa wasipelekwe makao makuu.
“Wale askari wadogo wanaofanya kazi vizuri msiwakatishe tamaa. Anamkamata mtu mnamwambia amwachie. Msisite kuleta mapendekezo kwa wale wanaofanya vizuri. Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri kama majeshi mengine lakini hizi dosari lazima zirekebishwe,” amesema.
Oktoba 2018, akiwa Jijini Dar es Salaam mfanyabiashara Mohemed Dewji alitekwa na watu wasiojulikana ambao walitajwa kuwa ni raia kutoka nje ya nchi lakini baadaye alipatakana maeneo ya Gymkhana Jiji Dar es Salaam.
Rais Magufuli Aonyesha Kutoridhishwa na Upelelezi wa Tukio la Kutekwa Mo Dewji
0
March 04, 2019
Tags