Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amekumbushia sakata la kutekwa mfanyabiashara Mohamed Dewji na kusema kuwa anashangaa kwanini mpaka sasa watu waliomteka hawakufikishwa mahakamani
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo Jijini Dar es salaam wakati wa zoezi la kuwaapisha Makamishna wa juu wa jeshi la polisi pamoja na mawaziri wapya wawili akiwemo Waziri wa Katiba na Sheria na Dkt Agustine Mahiga pamoja na Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Paramagamba Kabudi.
Rais Magufuli amesema, "Jeshi la Polisi linatakiwa kuelewa kuwa Watanzania sio wajinga, kama suala la kutekwa kwa Mo Dewji linaacha maswali, tuliambiwa alitekwa na wazungu lakini lilipoisha haikueleweka, mwishoni aliyetekwa alionekana anakunywa chai na Mambosasa."
"Tulioneshwa nyumba na dereva lakini hadi leo hakuna aliyepelekwa Mahakamani hata kama Watanzania watanyamaza lakini mioyo yao haitakuwa sawa", ameongeza Rais Magufuli
Oktoba 2018, akiwa Jijini Dar es salaam mfanyabiashara Mohemed Dewji alitekwa na watu wasiojulikana ambao walitajwa kuwa ni raia kutoka nje ya nchi lakini baadaye alipatakana maeneo ya Gymkhana Jiji Dar es salaam.