Idadi ya watu waliofariki kutokana na kimbunga Idai nchini Msumbiji sasa huenda ikawa ya juu na kufikia watu 1000 rais Filipe Nyusi amesema.
Bwana Nyusi alisafiri kwa ndege katika maeneo yalioathirika zaidi siku ya Jumatatu. Alielezea kuona miili ikielea juu ya mito.
Tayari kuna hatari ya maisha ya zaidi ya watoto 100,000 na watu wazima kufuatia kikmbunga hicho huku mito katika maeneo yaliothirika zaidi ikivunja kingo zake , kulingana na shirika la Save the Children.
Mafuriko yaliofanyika mapema mwezi huu yamezidishwa na kimbunga Idai ambacho kilikumba eneo la kaskazini mwa Msumbiji mnamo tarehe 15 mwezi Machi 2019 na kusababisha unahiribifu mkubwa wa nyumba , shule, hospitali na miundo mbinu.
Kulingana na serikali ya Msumbiji takriban watu 600,000 wameathiriwa , huku maisha ya zaidi ya watu 1000 yakidaiwa kupotea huku yale ya watu 100,000 yakihitaji msaada wa dharura mjini Beira.
Kiwango cha janga hilo kinazidi kuongezeka kila dakika na shirika la Save the Children lina wasiwasi mkubwa kuhusu watoto na familia walio katika hatari huku viwango vya mafuriko vikizidi kuongezeka anasema Machel Pouw mkuu wa operesheni ya shirika hilo nchini Msumbiji.
Save the Children ni mwanachama wa COSACA wakishirikiana na shirika la OXFAM pamoja na lile la CARE na linafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na serikali pamoja na taasisi za usimamizi wa majanga ili kuwasaidia watoto walioathirika
Kimbunga hicho kilishuka katika mji wa bandari wa Beira siku ya Alhamisi kikiwa na upepo wenye kasi ya hadi kilomita 177 kwa saa , lakini mashirika ya misaada yalifika katika eneo hilo siku ya Jumapili.
Mfanyikazi mmoja wa Umoja wa mataifa aliambia BBC kwamba kila nyumba mjini Beira- ambapo ni mji wenye makaazi ya watu nusu milioni iliharibiwa.
Gerald Bourke, kutoka kwa shirika la chakula duniani , alisema: Hakuna nyumba ambayo haikuathiriwa . hakuna Umeme, hakuna mawasiliano.
Barabara zimejaa magogo ya nyaya za umeme. Paa za nyumba zimeanguka pamoja na nyuta zake. raia wengi wa mji huo wamepoteza makaazi yao.
Idadi rasmi ya watu waliofariki nchini Msumbiji inadaiwa kuwa watu 84 kufuatia mafuriko na upepo mkali.
Kimbunga hicho kimewaua takriban watu 180 katika eneo lote la Afrika Kusini.
Shirika la msalaba mwekundu limeelezea uharibifu huo kuwa mbaya zaidi na wa kutisha. Watu wamelazimika kuokolewa wakiwa juu ya miti , Jamie LeSeur mkuu wa IFRC aliambia BBC.
Rais wa Msumbiji Asema Huenda Watu 1000 Wamefariki Kutokana na Kimbunga
0
March 19, 2019
Tags