Rita yasajili Bodi ya CUF inayomuunga mkono Lipumba

Rita yasajili Bodi ya CUF inayomuunga mkono Lipumba
Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, imepata usajili baada ya kukidhi vigezo vya kisheria.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu CUF, Magdalena Sakaya, alisema bodi hiyo imepata usajili baada ya kurekebisha kasoro mbalimbali zilizoelezwa na Mahakama Kuu, Februari 18 mwaka huu, jambo lililosababisha awali kushindwa kusajiliwa.

Akisoma barua ya Kaimu Katibu Ofi sa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufilisi na Udhamini (Rita), Emmy Hudson, kwenda kwa chama hicho, Sakaya alisema:

“Baada ya wakala huo kupitia nyaraka zilizowasilishwa na chama hicho kwa kuzingatia sheria ya usajili wa wadhamini sura 318, marejeo ya 202 kifungu cha 17 (1B) cha sheria ya Vyama vya Siasa na marekebisho yake.

“…pamoja na ofisi  ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuonyesha ushiriki katika kikao cha kuzingatia maelekezo ya hukumu, Mahakama Kuu ya mislenia civil case namba 13n ya 2017 mbele ya Jaji Masoud J., hivyo nimeridhika na nyaraka hizo baada ya kuonekana kuwa sahihi na zimehifadhiwa katika kumbukumbu za ofisi,” alisema Sakaya akisoma barua hiyo.

Aliwataja wajumbe tisa wanaounda Bodi hiyo kuwa ni pamoja na Peter Malebo, Hadra Silia, Aziz Dagesh, Abdul Magomba,
Amina Msham, Asha Suleiman, Mussa Kombo, Salha Mohamed na Suleiman Makame Issah.

“Nichukue fursa hii sasa kuwajulisha wananchi wote, wanachama wote wapenzi wote wa CUF popote walipo Bodi ya Wadhamini imesajiliwa na muda wowote kuanzia sasa Bodi itakaa kuweza kumchagua mwenyekiti wao ambaye ataongoza Bodi.

“Baada ya hapo wataweza kuangalia mambo yote ya chama kwa sababu kikatiba mambo mengi ya chama yanasimamiwa na bodi, ikiwamo kuangalia kesi zilizopo mahakamani, chama kimekwisha kuwa na bodi na anayeshtakiwa ni bodi, si mtu binafsi,” alisema.

Kutokana na hatua hiyo, Sakaya aliwataka wanachama na wapenzi wa chama hicho kuachana na kile alichokiita kuwa ni ‘blabla’ zinazoandikwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kwa lengo ya kuichafua CUF.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad