STAA wa Ureno, Cristiano Ronaldo, ameitwa kwa mara kwanza kwenye timu ya taifa ya nchi hiyo kuanzia walipoondolewa kwenye Kombe la Dunia.
Ureno hawakufanya vizuri kwenye Kombe la Dunia na uongozi wa soka wa nchi hiyo haukumuita Ronaldo kuanzia Julai mwaka jana, huku akiachwa azoee mazingira ya timu yake mpya ya Juventus.
Lakini juzi mshambuliaji huyo alifanya mazoezi na wenzake kwa mara ya kwanza akijiandaa na michezo miwili ya kutafuta nafasi ya kufuzu Euro mwaka 2020. Ureno walikuwa wakijifua kwenye eneo la Oeiras, karibu na jiji la Lisbon na mazoezi hayo yalionekana kuwa na mvuto mkubwa kutokana na uwepo wa mchezaji huyo ambaye ameshatwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia mara tano.
Mbali na Ronaldo wachezaji wengine ambao waliongeza mvuto kwenye timu hiyo ni Bernardo Silva wa Manchester City na wachezaji wanne kutoka Wolves.
Ureno wanajiandaa kucheza michezo miwili ya kufuzu kwa michuano hiyo dhidi ya Ukraine na Serbia ambayo itapigwa ndani ya wiki mbili. Mshambuliaji huyo wa Juventus ndiye kinara wa kufunga mabao kwenye nchi hiyo akiwa amefanikiwa kufunga mabao 85 kwenye michezo 154.
Wachezaji watano wameitwa kwenye timu hiyo wakitokea England ambao ni Ruben Neves, Joao Moutinho, Rui Patricio na Diogo Jota ambao wanaichezea Wolves na Silva wa Man City. Timu hiyo itaanza harakati zake dhidi ya Ukraine Machi 22 kabla hawajawakaribisha Serbia siku tatu.