Rwanda imewasihi wananchi wake kusitisha ziara na biashara nchini Uganda

Rwanda imewasihi wananchi wake kusitisha ziara na biashara nchini Uganda
Serikali ya Rwanda imewasihi wananchi wake kusitisha ziara zao nchini Uganda baada ya kuishtumu nchi hiyo kuwanyanyasa raia wake wanaoishi ama kutembelea nchini humo.

Uganda imeishutumu Rwanda kufunga mipaka baina ya nchi mbili,lakini Rwanda imekanusha na kusema mipaka iko wazi.

Alhamisi iliyopita mamlaka ya mapato ya Rwanda iliamrisha maroli ya mizigo kutotumia tena mpaka wa Gatuna kwa madai ya shughuli za ujenzi wa kituo kimoja cha mpakani 'one stop border' baina yake na Uganda.

Kwa mjibu wa mamlaka ya mapato ya Rwanda malori yaliombwa kutumia mpaka wa pili wa Kagitumba kaskazini mwa Rwanda.

Hata hivyo watumiaji wa mipaka hiyo miwili hupendelea njia ya mpaka wa Gatuna kuwa rahisi na fupi kuliko ya mpaka wa Kagitumba.

Nchi mbili zinaendelea kurushiana lawama.
Rwanda inaishutumu Uganda kunyanyasa wanyarwanda wanaoishi ama kufanyia biashara nchini Uganda na pia kuunga mkono makundi ya waasi hususani kundi la Rwanda National Congres linaloongozwa na mkuu wa zamani wa majeshi Jenerali Kayumba Nyamwasa aliyeko uhamishoni nchini Afrika kusini.

Kwa upande mwingine, Uganda inashutumu Rwanda kwa vitendo vya kijasusi kwenye ardhi yake huku ikiwashuku baadhi ya raia wa Rwanda kuhusika na vitendo hivyo.

Haki miliki ya pichaUGANDA MEDIA CENTRE
Mkwamo wa shughuli katika mpaka wa Rwanda Uganda.

Eneo hilo lina umuhimu mkubwa kibiashara kieneo.

Ni eneo ambalo huruhusu kupita kwa bidhaa kutoka mji mkuu wa Uganda Kampala, au Mombasa pwani ya Kenya.

Wakaazi hapo wanasema ni kama 'ghala kwa biashara kutoka maeneo hayo'.

Akizungumza na BBC, Diwani Abel Bizimana katika eneo la Kisoro anaeleza kwamba, 'Hali haijabadilika. Tunaathirika kama viongozi wa kieneo, kama jumuiya ya wafanyabiashara na wateja pia tunaowahudumia.'

Kutokana na matatizo ya kibiashara na udhibiti wa watu kutoka na kuingia katika eneo hilo, watu ambao kawaida huja kupokea bidhaa kutoka mjini na wilaya ya Kisoro sasa inaarifiwa hawaji tena, wakiwemo hata waendesha boda boda ambao pia wamesitisha shughuli zao.

Siku mbili kuu za soko katika eneo hilo, Jumatatu na Alhamisi, ambazo hushuhudiwa shughuli nyingi za kibiashara, 'sasa limekuwa kama jangwa', anaeleza diwani Abel.

Usafiri wa mabasi umepungua pakubwa, bidhaa zinaharibika.

Wafanyabiashara wanaobeba mihogo au samaki wanapata hasara katika mpaka kwasababu mali zinaharibika.

'Nilipofika mpakani, nilihisi harufu kali ya samaki waliooza katika eneo hilo' ameongeza Abel.

Wiki iliyopita, msemaji wa serikali ya Uganda Ofwono Opondo ameiomba Rwanda kuruhusu wafanya biashara kuingiza bidhaa ili kuepuka hasara na uhasama zaidi.

Kwa upande wake Waziri wa maswala ya kigeni wa Rwanda, Richard Sezibera amenukuliwa akidai kuwa serikali ya Uganda inawadhulumu raia wa Rwanda wanaoishi Uganda.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad