Rais wa shirikisho la soka nchini Kenya (FKF), Nick Mwendwa, ameweka wazi kuwa serikali ya Kenya inaanza utekelezaji wa ahadi yake ya kuwekeza zaidi ya shilingi 240 milioni zaidi ya bilioni tano za Tanzania kwenye michezo.
Mwendwa amesema Serikali imethibitisha kuwa wiki ijayo itaikabidhi timu ya taifa ya mpira wa miguu (Harambee Stars) kiasi cha shilingi milioni 50 za Kenya, zaidi ya bilioni moja za Tanzania ikiwa ni sehemu ya ahadi ambayo ilitolewa na serikali kupitia kwa makamu wa Rais William Ruto.
Rais Mwendwa amesema pesa hizo zitatumika kutekeleza shughuli za soka, ikiwa ni pamoja na kuandaa timu kwaajili ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2019 zinazofanyika Misri.
"Mpaka wiki ijayo wachezaji wakiripoti kambini tuna uhakika pesa zitakuwa kwenye akaunti yetu na tutawapatia wagawane wenyewe kwa usawa kisha sisi tuendelee na maandalizi ya fainali hizo'', amesema Mwendwa.
Aidha Mwendwa amefafanua kuwa wachezaji wa Harambee Stars watapata milioni 35 za Kenya, zaidi ya milioni 700 za Tanzania ambayo ni asilimia 70 ya pesa hizo zinazotolewa kwa awamu hiyo ya kwanza ambazo ni bilioni moja.
Akizungumza mwaka 2017, Makamu wa Rais William Ruto, aliahidi serikali yake ipo tayari kusaidiza michezo kwa kuwekeza zaidi ya bilioni 5 ambazo kiasi kingine kitatumika kuwapa kama zawadi wachezaji endapo watafuzu AFCON 2019 jambo ambalo wamefanikiwa.
Kenya ambayo ina pointi 7 ikiongoza Kundi F lenye timu za Ghana na Ethiopia imeshafuzu tayari hivyo itacheza mchezo wa kuamua nani awe kinara wa kundi hilo dhidi ya Ghana yenye pointi 6, Machi 23.