Serikali Yatoa Onyo kwa Viongozi wa Wizara
0
March 19, 2019
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa wizara, taasisi au mikoa kuacha mara moja tabia ya kuwatumia waandishi wa habari binafsi katika utekelezaji wa majukumu yao ya Kiserikali na kuwaacha wale ambao wameajiriwa na serikali katika ofisi zao kwa kazi hiyo.
“Kwanza tabia hii ni hatari kwa usalama wa taarifa za Serikali. Nitumie nafasi hii kukemea viongozi na watendaji wenye tabia za namna hii kuacha mara moja tabia hizo zisizo kinyume na matakwa ya maadili ya utumishi wa umma.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jumatatu, Machi 18, 2019, katika ufunguzi wa Kikao Kazi cha 15 cha Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano Serikalini, kinachofanyika katika ukumbi wa BOT jijini Mwanza. Kikao hicho kinahudhuriwa na Maafisa Habari na Mawasiliano takribani 400.
Katika kuhakikisha suala hilo linakomeshwa Serikalini, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo umpelekee majina ya kiongozi au mtendaji wa ngazi yeyote ile ambaye bila sababu zozote anawapuuza waliajiriwa na Serikali kufanya kazi hiyo.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatumia rasilimali nyingi kuajiri, kuanzisha, kuiendeleza na kuitunza kada ya maafisa habari Serikalini, hivyo, maafisa habari waliopo wapewe nafasi ya kutekeleza majukumu yao kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Waziri Mkuu amesema maafisa hao wanatakiwa wapewe ushirikiano na viongozi wa taasisi wanazozitumikia ili habari za utekelezaji wa Serikali ziwafikie wananchi badala ya viongozi na wataalamu wengine kukalia habari hizo. “Mawaziri na Wakuu wa Mikoa, simamieni Maafisa Habari kutimiza wajibu wao”.
Waziri Mkuu amesema anafahamu changamoto nyingine kwa maafisa habari ambazo husababishwa na viongozi au watendaji katika taasisi za umma na hasa katika ngazi za Wizara, Mikoa na Halmashauri za kutotambua mchango wa sekta ya habari katika maendeleo ya nchi.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema anazo taarifa za baadhi ya maafisa habari ambao wana vifaa vyote pamoja na ofisi nzuri zenye kuvutia lakini bado hawatimizi wajibu wao ipasavyo katika kutangaza shughuli za Serikali.
“Wengine hawajui shughuli zinazofanywa na Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na Wakuu wa Sekta kwa siku, wiki hata mwezi, Taasisi haina taarifa. Badilikeni, nenda mkakusanye taarifa na mzitoe hadharani”.
Tags