MBEYA: Simanzi ilitawala baada ya Samwel James Chacha (25) ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo cha Ualimu Tukuyu, Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya kufariki dunia wakati akiogelea katika Mto Kiwira hivi karibuni.
Tukio hilo lilitokea Machi 7 mwaka huu, saa 6:30 mchana ambapo shughuli ya kuutafuta mwili wake ilianza mara moja kandokando ya mto huo. Baadhi ya mashuhuda ambao waliomba majina yao yasiandikwe gazetini walisema marehemu alikuwa akiogelea katika mto huo lakini ghafla walimuona akitapatapa.
“Ni kwamba huyu jamaa alikuwa akiogelea na alionekana kuwa ni fundi wa kuogelea lakini ghafla alianza kutapatapa na kuomba msaada, haikuchukua hata sekunde kumi akazama majini na hakuonekana tena.
“Baada ya kutoonekana, hali ya mashuhuda ikawa tofauti kwani watu wakawa wanasema ‘amezolewa…, amezolewa,’ na kweli hakuibuka tena,” alisema shuhuda huyo na kuongeza: “Wananchi pamoja na baadhi ya wanafunzi wenzake walionekana kupaniki lakini walishirikiana kuutafuta mwili wake, hata hivyo haukuonekana licha ya jitihada kubwa kufanyika.
“Siku ya nne tukapata taarifa kuwa mwili wake umepatikana katika Kijiji cha Mboyo, maana yake ni kwamba ulisombwa na kusafirishwa na maji hadi katika kijiji hicho wilaya ya Rungwe kutoka hapa Tukuyu.” Mwili huo ulipatikana Machi 11 mwaka huu saa 10:00 jioni katika Kijiji cha Mboyo, Kata ya Lupepo, Wilaya ya Rungwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Ulrich Matei alipozungumza na mwandishi wetu alisema ni kweli mwanafunzi huyo ambaye sasa ni marehemu alipoteza maisha na kifo kilitokana na kuogelea bila kuchukua tahadhari.
Aidha alisema baada ya mwili kuonekana Kijiji cha Mboyo polisi walikwenda na kuuchukua kisha kuupeleka kuhifadhiwa katika Hospitali ya Makandana kwa uchunguzi zaidi. “Nitoe wito kwa wananchi kuchukua tahadhari pindi wanapoogelea, pia watu wawe makini na watoto hasa katika kipindi hiki ambacho kuna mvua zinazoendelea,” alisema Kamanda Matei.