Taarifa Ya Jeshi La Polisi Kutoka Mkoa Wa Mbeya

Mnamo tarehe 12.03.2019 majira ya saa 20:00 usiku huko katika Kitongoji cha Mapogoro, Kijiji cha Kapunga, Kata ya Itamboleo, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya, CATHERINE MFIKWA [32] Mkazi wa Kapunga pamoja na mtoto wake aitwaye PRISCAN PIUS @ MWAFWALO [14] Mkazi wa Kapunga walijeruhiwa kwa kubabuliwa na moto sehemu za miguu yao kutokana na moto uliozuka ghafla kwenye duka lao.

Katika tukio hilo moto huo ulisababisha uharibifu wa bidhaa zilizokuwa zinauzwa kwenye maduka ya (1) PIUS AIDAN @ MWAFWALO [41] Mkazi wa Kapunga, aliyekuwa anauza vinywaji baridi (2) JOMBAA @ RAS aliyekuwa anauza vitu vya jumla (3) JUMA MWAMJINGA aliyekuwa anauza bidhaa za dukani na mahindi.

Majeruhi wamelazwa na wanapata matibabu katika Hospitali ya Misheni Chimala na wanaendelea vizuri. Bidhaa zote zilizokuwa zipo stoo zimeokolewa na zimekabidhiwa kwa wamiliki. Chanzo cha ajali hiyo ya moto ni kulipuka kwa jiko la gesi lililokuwa linatumiwa na CATHERINE MFIKWA (mke wa PIUS AIDAN @ MFIKWA) na kushika kwenye bidhaa za dukani na kusambaa kote. Moto huo umezimwa na kikosi cha zimamoto na uokoaji Wilaya ya Mbarali, Polisi na wananchi. Thamani ya mali iliyoungua bado kufahamika.

AJALI YA GARI KUGONGA UZIO NA NYUMBA NA KUSABABISHA MAJERUHI.
Mnamo tarehe 12.03.2019 majira ya saa 14:00 mchana huko maeneo ya Inyala, Wilaya ya Kipolisi Mbalizi, Mkoa wa Mbeya katika barabara ya Mbeya/Iringa, gari no. T. 608 DNP/T. 214 DNW aina ya FAW iliyokuwa ikitokea mkoa wa Songwe kuelekea Dar-es- Salaam ikiwa inaendeshwa na dereva asiyefahamika iliacha njia na kugonga uzio na nyumba inayotumika kwa huduma ya vipimo vya magonjwa mbalimbali ya binadamu [kliniki] na kusababisha majeruhi kwa 1. ZAKARIA CHINA [24] Mkazi wa Uyole ambaye ni mhudumu katika kliniki hiyo, 2. ELIUD FUNGO [38] Mkazi wa Inyala

ambaye ni Daktari wa kliniki hiyo 3. MAGRETHI HASSAN [32] Mkazi wa Inyala aliyekuwa anapata huduma 4. PILI MWANGAMBA [28] Mkazi wa Tunduma na alikuwa abiria kwenye gari hilo. Majeruhi wote wamepata majeraha ya kawaida mwilini na wamelazwa Kituo cha Afya Inyala. Chanzo cha ajali ni ubovu wa gari. Gari hiyo ilikuwa imebeba mzigo aina ya shaba. Msako mkali wa kumtafuta Dereva na mmiliki wa gari unaendelea.

KUFANYA SHUGHULI ZA UGANGA BILA KIBALI (LAMBALAMBA)
Mnamo tarehe 12.03.2019 majira ya saa 07:00 asubuhi huko katika Kijiji na Kata ya Sangambi, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Askari wakiwa katika msako waliwakamata 1. PETER DAUDI [37] Mkazi wa Mlimanjiwa 2. SIMON PAMBO [44] Mkazi wa Sangambi 3. AZOLE MWANAHELA [31] Mkazi wa Sangambi na 4. MASUMBUKO CHARLES @ MWANAHELA [36] Mkazi wa Sangambi wakiwa wanafanya shughuli za uganga wa lambalamba isivyo halali. Watuhumiwa walikamatwa wakiwa na madawa mbalimbali ya kienyeji, manyanga na ngoma mbili. Watuhumiwa wengine walitoroka kabla ya kutiwa nguvuni na juhudi za kuwasaka zinaendelea.

TAARIFA YA KIFO – RUNGWE.
Mnamo tarehe 07/03/2019 saa 12:30 mchana huko katika Mto Kiwira uliopo Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya Mwanafunzi wa Chuo cha Ualimu Tukuyu Mwaka wa Tatu aitwaye SAMWEL JAMES CHACHA [25] alikufa maji akiwa anaogelea kwenye Mto huo na mwili wake kutoonekana baada ya kusombwa na maji.

Kutokana na tukio hilo zilifanyika jitihada za kuutafuta mwili wa mwanafunzi huyo ambapo tarehe 11/03/2019 majira ya saa 16.00 jioni huko katika Kijiji cha Mboyo, Kata ya Lupepo, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe na Mkoa wa Mbeya kwenye mto kiwira mwili wa mwanafunzi huyo ulipatikana.

Chanzo cha tukio ni uzembe wa marehemu kutaka kuogelea kwenye mto huo bila kuchukua tahadhari. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Rungwe – Makandana kusubiri uchunguzi wa kitabibu. Upelelezi unaendelea.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa tahadhari kufuatia matukio ya kufa maji yanayosababishwa na uzembe wa kutovaa maboya wakati wanapoingia majini, mtoni au ziwani. Aidha kufuatia mvua zinazonyesha nawasihi wazazi kuwapeleka watoto wadogo shuleni na kuwapokea ili kuwalinda dhidi ya madhara ya kutumbukia katika maji.

KUZINI NA MAHARIMU.
Mnamo tarehe 09.03.2019 saa 21:00 usiku huko Mtaa wa Ghana, Tarafa ya Sisimba, Jiji na Mkoa wa Mbeya TUMAINI MWASOMI, Mkazi wa Mama John aligundua kubakwa kwa binti yake aitwaye CAREEN BONIPAHCE [14] Mkazi wa Ghana, Mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari LEJIKO na baba yake mzazi aitwaye BONIPHACE JULIUS [42] Mkazi wa Ghana.

Aidha CAREEN BONIPHACE anaishi Ghana na baba mzazi baada ya kutengana na mama yake na ndipo baba yake akaanza kumbaka mara kwa mara tangu Septemba, 2018 bila kumwambia mtu yeyote na ndipo juzi tarehe 09.03.2019 majira ya saa 21:00 usiku baba yake alitaka kumbaka tena na ndipo binti huyo alikataa na baba yake alianza kumpiga na kumsababishia maumivu makali mwilini na hivyo kupelekea kumsimulia shangazi yake aitwaye LUCY MWASUMBULE juu ya vitendo vya kubakwa anavyofanyiwa na baba yake.

Chanzo cha tukio ni tamaa za kimapenzi. Mtuhumiwa amekamatwa na yupo mahabusu. Mhanga anaendelea na matibabu Hospitalini.

KUPATIKANA NA MICHE YA BHANGI.
Mnamo tarehe 10.03.2019 saa 07:00 asubuhi huko eneo la Mapanga, Kijiji cha Stamiko, Kata ya Mkola, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi walikamata miche 30 ya bhangi ikiwa imelimwa kwenye shamba la mahindi lenye ukubwa wa robo heka mali ya NDUSHI SHIJA. Mtuhumiwa alikimbia na juhudi za kumtafuta zinaendelea lakini GUMBA ZALA [32] mkazi wa mapanga-stamiko ambaye ni mke wa mtuhumiwa na LUHENDE SHIJA [18] ambaye ni mtoto wa mtuhumiwa wamekamatwa kwa mahojiano. Mtuhumiwa ni mkulima na muuzaji wa bhangi. Upelelezi unaendelea.

MALI YA KUOKOTA.
Mnamo tarehe 10.03.2019 saa 21:30 usiku huko Kitongoji cha Lubele, Kata ya Ikimba, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi wakiwa doria pamoja na kikundi cha ulinzi shirikishi waliona gari aina ya Toyota Ractics rangi nyeupe ikiwa imeegeshwa maeneo ya uchochoroni kwenye pagala na watu wasiofahamika ambapo msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa unaendelea. Watuhumiwa waliacha gari hilo.

Baada ya kulikagua iligundulika kubomolewa kioo kidogo cha mbele upande wa dereva na pia kuharibika mfumo wa kuwashia gari, hivyo kuunganisha nyaya kwa urahisi wa kuliwasha. Gari hilo lilikuwa limebandikwa namba za kitanzania T 512 DCL na ndani ya gari hilo kumekutwa nyaraka zinazoonyesha kuwa ni IT iliyokuwa ikielekea Blantyre nchini Malawi. Ufuatiliaji unaendelea

KUPATIKANA NA MALI ZIDHANIWAZO ZA WIZI.
Mnamo tarehe 10.03.2019 saa 10:00 asubuhi huko maeneo ya ZZK Mbalizi na maeneo mbalimbali ya Mbalizi Wilaya ya Kipolisi Mbalizi. Askari Polisi wakiwa katika msako wa wahalifu na uhalifu na matukio ya uvunjaji walimkamata GOODLUCK JOSHUA [21] mkazi wa Nsalala akiwa na speaker mbili kubwa aina ya Dynamic Ailiong na Equalizers 1 aina media com na baada ya mahojiano alikiri kuhusika katika matukio mbalimbali ya uvunjaji na kutaja washiriki wenzake ambao ni JOHN MBEMBEJA, RAMADHANI, BONKE JIRANI na EMMANUEL MAPUNDA wote wakazi wa Mbalizi.

Makazi yao yamefanyiwa upekuzi na kupatikana mali mbali mbali ambazo ni:-
Mashine ya kuchezea bahati nasibu ya kichina 1,
Monitor aina ya dell 1,
CPU aina ya hp 1,
Radio za aina ya sub woofer zenye majina mbalimbali 5 na speaker zake 8,
King’amuzi cha kampuni ya startimes 1,
Mashine za kunyolea nywele aina home cut 2,
Cable ya umeme aina tronic 1,
Deck ya cd aina singsung 1,
Keyboard na mtungi mdogo wa gas kampuni ya Orexy,
Burner, pamaoja na stand yake mali zote zikidhaniwa kuwa za wizi.

Baadhi ya mali zimetambuliwa katika matukio ya uvunjaji. Mbinu ni kuvunja makufuri ya maduka na sehemu za biashara nyakati za usiku na kuiba

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad