MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar, imeutaka upande wa serikali ambao ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuharakisha upelelezi wa kesi ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura.
Wambura anakabiliwa na mashitaki 17 likiwemo shitaka la kughushi nyaraka na utakatishaji fedha ambapo mashitaka hayo hayana dhamana.
Wakili wa Wambura, Majura Magafu, jana Alhamisi aliiambia mahakama kuwa upande wa serikali unatakiwa kuwasilisha ushahidi wao kwa sababu mpaka wamemkamata mshitakiwa ina maana kila kitu kipo tayari.
Aidha, wakili wa serikali, Wankyo Simon, aliiambia mahakama kuwa upelelezi bado haujakamilika na anaomba wapangiwe tarehe nyingine kusikiliza shauri hilo.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Kelvin Mhina, aliutaka upande wa serikali kuharakisha upelelezi wa kesi hiyo kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Baada ya kutolewa agizo hilo, hakimu akaahirisha kesi hiyo mpaka Machi 14, mwaka huu.