Ukisikia Mwanaume Kuwa na Koromeo Ndiyo Huku


MWANAUME ame umbwa na koromeo. Ndiyo sentesi utakayoisikia mitaani kunapokuwa na mjadala unaohusisha suala la uvumilivu, kubeba siri na kukubaliana na matokeo yoyote! Kwamba inaaminika mtoto wa kiume hakuna kinachomshinda chini ya jua.

Kuna ukweli katika hilo, lakini baadhi ya wanaume hutuangusha kwa kushindwa kuwa na sifa hizo. Wakati fulani mwanaume anaweza kulevywa na penzi la mwanamke kiasi cha kukabidhi sifa zake hizo kwake.

Tunakumbuka kisa cha Samsoni na Delila kwenye Biblia. Samsoni alijikuta akitoa siri za nguvu zake kwa kumweleza Delila ambaye aliuza dili kwa Wafilisti, wakaja kumkamata baada ya kunyolewa nywele zake – zilizokuwa siri ya nguvu zake.

Samsoni alileweshwa na penzi. Usiwe kama Samsoni. Wakati fulani unaweza kutofautiana na mkeo au mchumba wako, halafu unaona suluhu ni kupeleka jambo lako kwa watu wengine! Unafeli sana mzee.

Jiulize, hadi wewe upeleke mambo yako kwa rafiki yako, kwani yeye hagombani na mwanamke wake? Kumbuka binadamu tumetofautiana . Inawezekana upo na mpenzi au mkeo, lakini kuna watu hata walio karibu yako wanamtolea macho. Sasa ikitokea bahati mbaya umepeleka jambo lako kwa mtu wa namna hiyo, maana yake umeeleza udhaifu wako na wa mwanamke wako.

Si ajabu akatumia nafasi hiyo, kukuovateki na kukuchukulia mpenzi wako kiulaini. Tusisahau ndugu zangu, tuliagizwa tuishi nao kwa “akili”. Hata kama kuna jambo kubwa kiasi gani limetokea kwa mwenzi wako, kwanza tumia koromeo lako vizuri.

Kunywa maji. Tulia, kisha tafakari. Mwanaume ana akili ndefu, asikudanganye mtu. Hakuna jambo lolote linaloweza kuishinda akili ya mwanaume. Ni suala la kuamua na kutenda. Hakuna kitu kipya utakachosaidiwa na rafiki yako. Mwanaume kamili mwenye koromeo, atajiuliza mwenyewe, “Hivi nakosea wapi?” au “Mwenzangu anakosea wapi?”

Kwa kujiuliza maswali hayo kwa utulivu ni rahisi kupata majawabu ambayo yatakusaidia kukaa chini na mwenzako kisha kurekebisha hali ya hewa. Unadhani basi wanawake wana tabu? Hawana… ni sisi wenyewe sometimes tunajichanganya.

Mwanamke akishakula akashiba, akalala mahali pazuri, akavaa vizuri, ukaonyesha kumjali kwa kumfanyia vimahaba vya hapa na pale, unamalizia na jambo moja tu la mwisho kikamilifu. Mchezo umeisha.

Wakati mwingine unalalamika mkeo ni mkorofi, kumbe kuna mahali unafeli. Angalia vizuri hayo niliyosema hapo juu, unayatimiza? Mkeo ana uhakika nayo kutoka kwako? Nakuhakikishia ukitimiza hayo, bila kusahau lile la mwisho; kikamilifu, mkeo atakuwa mtulivu hadi utashangaa.

Nakuambia mzee mwenzangu, maliza mambo yako mwenyewe. Ukitumia akili yako vizuri, mwanamke hana shida kabisa. Utagundua kuwa kumbe ndoa ni paradiso ndogo ya huku duniani. Kama unabisha anza kutumia koromeo lako leo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad